July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Taifa Stars wanaanza kujiwinda kuikabili Malawi

Spread the love

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kimeanza mazoezi leo mchana katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo dhidi ya Malawi utakaocheza Jumatano Oktoba 7, 2015, kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Taifa Stars inayonolewa na kocha mkuu mzawa, Charles Mkwasa akisaidiwa na Hemed Morroco, Peter Manyika na mshauri wa Ufundi, Abdallah Kibadeni wameingia kambini jana katika hoteli ya Urban Rose iliyopo Kisutu jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wote wameripoti kambini isipokuwa wachezaji wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mrisho Ngassa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaotarajiwa kuungana na wenzao mwishoni mwa wiki baada ya kumaliza michezo inayowakabili wikiendi hii.

Wachezaji waliopo kambini ni magolikipa Ali Mustafa, Aishi Manula, Said Mohamed, walinzi Juma Abdul, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani na Nahodha, Nadir Haroub “Cannavaro”.

Wengine ni viungo Himid Mao, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Said Ndemla, Salum Telela, Deus Kaseke, Saimon Msuva, Farid Musa, washambuliaji John Bocco, Rashid Mandawa na Ibrahim Hajibu

Wakati huohuo, Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ imethibitisha kushiriki michuano ya timu za Taifa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Chalenji) itakayofanyika nchini Ethiopia kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 6, 2015.

Michuano ya CECAFA Chalenji ndio michuano mikongwe zaidi barani Afrika ambapo jumla ya nchi 12 wanachama hushiriki michuano hiyo iliyofanyika mara ya mwisho mwaka juzi nchini Kenya na wenyeji kutwaa ubingwa huo.

Nchi wanachama wa CECAFA ni Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somalia, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.

error: Content is protected !!