October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Taifa njia panda

Spread the love

UCHAFUZI uliofanywa na wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa, umelifikisha taifa njia panda. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kauli mbalimbali zinazoashiria kuharibika kwa uchaguzi huo, kutoka kwa wanasiasa, viongozi wa dini na hata wanaharakati, zimetolewa baada ya vyama vya upinzani kujitenga.

Tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha ACT-Wazalendo, Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha Umma (Chaumma), vimetangaza kujiondoa kwenye uchaguzi huo huku Chama cha Wananchi (CUF), kikieleza kutafakari ushiriki wake.

Jana tarehe 10 Novemba 2019, Selemani Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), aliagiza walioondolewa warejeshwe.  Alitoa kauli hiyo jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Chadema kimewataka wagombea wake kupuuza wito huo na kueleza, kwamba kimejiondoa kudhamini mgombea yeyote ambaye miongoni mwa sharti la kugombea, lazima atokane na chama cha siasa.

Pia kimepiga marufuku kutumika kwa nembo ya chama hicho kwenye karatasi za uchaguzi huo, kwa kuwa tayari kimetangaza kujitoa na kina haki hiyo.

John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara akizungumza na wanahabari jana amesema, dhuluma zinazofanywa na wasimamizi zimekisukuma kujitoa na sasa wanaiandikia barua serikali ili kuweka kumbukumbu sawa.

“Sisi kama Chadema tutamwandikia barua Waziri Jafo ya kumpiga marufuku kulitumia jina la Chadema au nembo yake katika mchakato wa uchaguzi kwasababu tumejitoa,” amesema Mnyika.

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo amesema, kulingana na hali ilivyo sasa na kiwango kikubwa cha hujuma, ipo sababu ya kuelekeza nguvu katika kudai Tume Huru ya Uchaguzi huku akituhumua CCM kushiriki.

“Jambo moja tumejifunza kwenye mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kuwa, CCM imedhamiria kutumia dola kuiba uchaguzi wa mwakani.

“Huu wa sasa ulikuwa ni experimentation (majaribio). Sasa Vyama vya Siasa tutajikita kutaka Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini.

Ismail Jussa, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mikakati, usimamizi na ufuatiliaji wa ACT-Wazalendo amesema, “La kuvunda halina ubani!

“Uchaguzi huu umekorogeka na umepoteza uhalali. Ili kuiepusha nchi na mifarakano, suluhisho ni kuanza upya kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa ili kukubaliana namna bora ya uendeshaji na usimamizi wake. Hakuna njia ya mkato.”

Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki ameshauri, kwamba kwa kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019, tayari umeharibika, utafutwe muafaka wa haraka.

“Kinachohitajika kufanyika: Kanuni mpya za uchaguzi zitungwe kwa maridhiano na makubaliano ya vyama vinavyoshiriki. Utaratibu wa usimamizi wa uchaguzi kuanzia utoaji na upokeaji wa fomu, kushughulikia mapingamizi, kampeni na kutangaza matokeo uridhiwe na kukubaliwa na vyama,” amesema Lissu na kuongeza;

“Waziri wa TAMISEMI Selemani Jaffo amefuta maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi ya kuwaengua wagombea wa upinzani nchi nzima.

“Lakini Waziri Jaffo hana mamlaka ya kisheria ya kufuta maamuzi hayo. Yaliyotokea na yanayotokea ni ushahidi kwamba uchaguzi huu umeshaharibika. Haurekebishiki.”

Dk. Fredrick Onaeli Shoo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ameshauri kutendwa haki kwa vyama vyote vya siasa.

“Msimamizi mkuu wa uchaguzi anayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa vyama vyote. Zoezi hili lisipofanyika kwa haki, linaweza kusababisha fujo na uvunjifu wa amani. Wito wangu kwake na wasimamizi wengine wote wasimamie haki,” amesema Dk. Shoo.

error: Content is protected !!