August 2, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Taharuki ugonjwa wa Maalim Seif

Spread the love

AFYA ya Maalim Seif Sharif Hamad imeibua taharuki bara na visiwani huku wananchi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) wakisubiri taarifa kamili, anaandika Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Jana Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF alilazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uchovu.

Maalim Seif, aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana visiwani Zanzibar, alilazwa kwenye hospitali hiyo ikiwa ni siku tatu tu baada ya kutoka nchini India kupata matibabu ya upasuaji wa mgongo.

Licha ya Nassoro Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar kusema kwamba, chanzo cha Maalim Seif kulazwa katika hospitali hiyo jana asubuhi ni uchovu wa safari yake ya India, wananchi hapa visiwani wanaonesha wasiwasi wao kutokana na hali yake hasa wakati huu ambapo kuna mkwamo wa kisiasa visiwani humo.

“Bado tuna mashaka, tunapenda Mungu amjaalie afya njema zaidi ili aweze kupambana vizuri na hili wimbi la Chama Cha Mapinduzi ambao tayari wameonesha njia ya kupoka uamuzi wa Wazanzibari kwenye uchaguzi uliopita,” anasema Salim Said Rajabu wa Zanzibar na kuongeza;

“Matukio kama haya kuwapata watu muhimu hasa kwenye wakati huu, yanaibua hisia tofauti kabisa. Mungu atuepushe na hila za viongozi wa CCM ambao kwao wanaweza kufanya chochote ilimradi tu wakidhi matakwa yao.”

Hata hivyo, Abdul Kambaya, Naibu Mkurugnzi wa Mawasiliano na Umma CUF ameuambia mtandao huu leo kwamba, wananchi wanapaswa kuondoa hofu.

“Najua hofu hiyo ipo, si Zanzibar pekee hata huku bara wanapata hisia hizo kwa kuwa michezo ya kisiasa ni migumu, lakini tunaamini kwamba kwa Maalim Seif ni hali ya kawaida tu kama mwanadamu.

“Tunapaswa kuwa na imani kwamba, Malim Seif anaumwa kama viumbe wengine, tena anaweza kuumwa wakati wowote kwa namna Mungu atakavyotaka lakini cha msingi ni kumwombea kwa Mungu.”

Akizungumzia hali ya Malim Seif, Kambaya amesema, hana tatizo kubwa kama watu wanavyoweza kufikiri na kwamba, kwa sasa anaendelea vizuri.

“Ni kama alivyoeleza Marzui jana kwamba anaendelea vizuru, hali hiyo mpaka sasa anayo,” amesema na kuongeza;

“Anaweza kujifanyia mambo yote mwenyewe na wala hahitaji msaada kama mgonjwa. Kapumzika vya kutosha na ninaamini ataendelea na majukumu yake yaliyomleta hapa kama kawaida.”

Baada ya kulazwa jana, Mazrui alieleza kuwa, “jioni hii (jana) nimeongea naye, anakula kila kitu, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya ya Maalim Seif.”

Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini jana walikwenda kumjulia hali.

error: Content is protected !!