September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TaESA yaonya wafanyao kazi nje ya nchi

Afisa habari wa TaESA, Jamila Mbarouk

Spread the love

WAKALA wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) imewataka Watanzania kutokubali kusafirishwa pia kuajiriwa nje ya nchi pasipo kufuata taratibu za kisheria, anaandika Happiness Lidwino.

Pia, Watanzania wametakiwa kuwa makini na mawakala binafsi ambao huwatafutia kazi bila kufuata utaratibu ambapo hufanya hivyo kwa kujinufaisha wenyewe.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar ers Salaam na Jamila Mbarouk Afisa habari wa TaESA ambapo amesema, Watanzania wengi wamekuwa wakikimbilia kuajiriwa nje ya nchi baada ya kupata nafasi kutoka kwa mawakala binafsi bila kupitia TaESA kwa ushauri wa kisheria hali inayowafanya kutotambua haki zao za msingi wawapo huko.

Amesema, Watanzania wengi hawaelewi wapi pakuanzia pindi wanapopata ajira nje ya nchi hivyo kusaini mkataba ambao unawakandamiza wanapokuwa katika sehemu za kazi.

Mbarouk amesema, ili kuepuka adha hiyo ni vyema mawakala wa ajira na wanaotafutiwa ajira kuwaona TaESA kwa ushauri wa kisheria na mambo mengine muhimu ambayo wanapaswa kufahamu kabla ya kwenda nje ikiwa ni pamoja na maslahi yao.

Pia amesema, hadi sasa wamewasaidia watu zaidi ya 20,000 kupata ajira ndani na nje nchi na kuongeza kuwa , wameandaa semina kwaajili ya wanavyuo ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto ya soko la ajira nchini.

Pamoja na kuwasaidia watu hao TaESA inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuwatafutia watu ajira ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu kuliko mahitaji, waomba kazi kuwa na matarajio makubwa zaidi ya uhalisia hivyo kushindwa kupata nafasi.

“Mtu anaomba kazi anatarajia ajenge nyumba na kununua gari ndani ya miezi sita kitu ambacho hakipo na haiwezekani kwahiyo linapokuja suala la malipo inakuwa ngumu kukubaliana”amesema Mbarouk.

Mbarouk amesema, changamoto nyingine kuwa ni waajiri wengi kuhitaji watu wenye uzoefu wa miaka mingi katika nafasi wanazoomba, kutokujiamini na wengine kukosa sifa wakati wa usahili.

error: Content is protected !!