January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TACCEO yamshangaa Rais Kikwete

Spread the love

MTANDAO wa asasi za kiraia wa kuangalia chaguzi Tanzania (TACCEO) umeeleza kumshangaa Rais Jakaya Kikwete kwa kuteua watendaji wapya ikiwa zimebaki siku chache kabla ya taifa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Julai 25 mwaka huu Rais Kikwete alimuondoa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba, baada ya hapo alimwondoa Mkurugenzi wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa NEC, Dk. Sisti Cariah, pia aliwateua makamishna wawili wapya. Yoye haya yalifanyika ndani ya miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Makamishna walioteuliwa hivi karibuni ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mary Longway na Wakili Asina Omari.

TACCEO ambao pia unaratibiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) umeeleza kwamba, kitendo hicho kinaweza kusababisha mkanganyiko katika utendaji kutokana na makamisha hao kuwa wapya kutokuwa na uzoefu katika majukumu hayo.

Akizungumzia na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TACCEO, Wakili Imelda Urio amesema, hatua hiyo inaweza ‘kutibua’ utulivu uliopo sasa.

“Hatua hiyo inaweza kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu na kuwanyima wananchi haki zao za msingi kutokana na uongozi kubadilika na kurudisha nyuma baadhi ya mambo. Ingependeza watumishi walioanza ndio wangemaliza hadi mwisho,” amesema Urio.

Mbali na hilo, Urio amesema bado wanashangazwa na kitendo cha NEC kutoweka hadharani Daftari la Kudumu la Wapiga Kura huku zikiwa zimesalia siku 18 Watanzania wakapige kura. Wapo baadhi ya wana-vyuo ambao bado hawajajua watapiga kura katika vituo gani kwa kuwa wengi wao walijiandikisha sehemu tofauti.

“Tumeshuhudia changamoto nyingi sana wakati wa kujiandikisha na wengine hadi sasa majina yao hayapo kwenye orodha ya wapiga kura. Changamoto hizo na nyinginezo zinaleta mashaka kwa baadhi wa wananchi wanaweza kukosa haki zao za msingi kwa kutipiga kura. Tunaomba tume iangalie hilo,” amesema Urio.

Amesema, kifungu cha 11A na 22 cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 kinaitaka NEC kuweka daftari lenye orodha ya wapiga kura hadhalani ili kutoa fursa na haki kwa wananchi kuweka pingamizi kwa wale wasio kidhi vigezo.

“NEC inatakiwa kuondoa huu mkanganyiko unaoweza kujitokeza katika vituo vya uandikishaji wa wapiga kura na vituo vya kupiga kura kwani watu walijiandikisha katika vituo mbalimbali kama ofisi za serikali za mitaa hivyo inatakiwa ifahamike mapema ni vituo gani vitakavyotumika,” anasema.

Aidha, TACCEO inashiriki uangalizi wa uchaguzi mkuu kwa lengo la kutazama jinsi Tanzania inavyoheshimu haki ya kupiga kura na haki za wananchi kushiriki shughuli za umma kama ilivyoainishwa kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

error: Content is protected !!