June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tacaids yatoa tathmini ya mwitikio wa Ukimwi

Spread the love

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) kwa kushirikiana na Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) imetoa ripoti inayoonesha tathmini ya mazingira ya kisheria katika mwitikio wa Ukimwi nchini. Anaandika Regina Mkonde  (endelea).

Ripoti hiyo inawasilisha matokeo ya utafiti wa kina wa Tathmini ya Mazingira ya Kisheria kuhusu Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) nchini (Tanzania Bara na Zanzibar).

Tathmini imefanywa kwa lengo la kubaini sheria zilizopo pamoja na upungufu katika mfumo wa sheria na kanuni za nchi zinazohusiana na udhibiti wa Ukimwi kwa ujumla kwenye ngazi mbalimbali za utekelezaji.

Aidha, tathmini imeangalia jinsi sheria za nchi zinavyosaidia au kurudisha nyuma juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Ali Salim Ali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, amesema ripoti iliyotolewa inachambua sheria, sera na kanuni zinazohusiana na VVU na Ukimwi kwa lengo la kuona jinsi wananchi wanavyopata haki ya huduma muhimu za Ukimwi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

“Tunataka kuona jinsi haki hizo zinavyothaminiwa na kulindwa hususan kwa makundi maalum katika jamii yaliyo kwenye hatari ya kupata maambukizi mapya ya VVU,” alisema Dk. Ali.

Amesema ripoti inaonesha kiwango cha uhamasishaji, uelewa na kufuatwa kwa sheria zinazohusiana na VVU na Ukimwi na pia kuangalia jinsi wahusika hasa wabunge, wasimamizi wa sheria na watoa huduma za afya wanavyofuata matakwa ya sheria wakati wa utekelezaji na utoaji huduma zinazohusiana na VVU na Ukimwi.

“Tathmini iliyofanywa inatoa mapendekezo ya jumla ya nini kifanyike kwenye sheria na kanuni ambazo ni nyenzo muhimu katika kuboresha mwitikio wa Ukimwi,” amesema Dk. Ali akiongeza kuwa tathmini ilifanywa mikoa 11 ya Tanzania Bara ambayo ni Tabora, Katavi, Shinyanga, Mara, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Rukwa, Njombe, Iringa na Ruvuma.

Kwa Zanzibar, tathmini hiyo ilihusu mikoa yote mitano ya Zanzibar – Kusini, Kaskazini na Mkoa wa Mjini Magharibi kwa Unguja, na Kusini na Kaskazini kwa kisiwani Pemba.

Utafiti ulitumia nadharia ya haki za binadamu na kufanyika katika hatua sita ambazo zilijumuisha mapitio ya majarida, utafiti halisia uliojumuisha udahili wa makundi na watu mbalimbali, majadiliano kupitia vikundi, uandishi wa ripoti, mapitio ya ripoti katika ngazi mbalimbali hatimaye kuhaririwa na kupitishwa.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tacaids, Elizabeth Kaganda alieleza matokeo muhimu ya utafiti ikiwa ni pamoja na utungwaji wa sheria maalum za VVU na Ukimwi, uanzishwaji wa vituo vya utoaji wa huduma za upimaji na tiba kwa kutoa dawa za kupunguza makali ya VVU.

“Zimetungwa sheria maalum za VVU na Ukimwi, hata hivyo idadi kubwa ya watu hawana uelewa wa sheria hizi ama haki za watu wanaoishi na VVU au waliopata athari mbalimbali kutokana na VVU auUkimwi,” alisema Kaganda.

Kaganda alisikitishwa na baadhi ya taratibu za utoaji wa huduma zinazolenga kuongeza huduma za VVU naUkimwi zinazochochea unyanyapaaji na ubaguzi hasa wanawake wajawazito wanaoishi na VVU kuhudumiwa sehemu tofauti na wanawake wengine.

Ameitaka serikali kuhakikisha sheria za Ukimwi za pande zote mbili zinatangazwa ili zieleweke kwa jamii na kuchukua majukumu katika utekelezaji wa haki zilizo ainishwa kwenye sheria hizo.

error: Content is protected !!