Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Tabia zao huumba taswira zao
Makala & Uchambuzi

Tabia zao huumba taswira zao

Picha kubwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli
Spread the love

IMEKUWA utaratibu uliozoeleka maeneo mengi duniani, kwamba kila kiongozi wa nchi anapoingia madarakani vyombo vya habari humpachika jina “jepesi,” mbali na majina yake rasmi. Anachambua Maguha Maligisu … (endelea).

Vyombo hivyo vya habari, hufanya hivyo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo wepesi wa kutamkika, kuandikika na hata “kushikika” kirahisi.

Magazeti hasa ndiyo hujipa kazi hii, kuliko vyombo vingine vya kielektroniki; redio na televisheni. Haya hufanya hivyo, mara nyingi, kuweza kubeba majina marefu kwenye magazeti yao.

Mifano ya Tanzania inaweza kuthibitisha hoja hii; kwamba alipoingia madarakani Jakaya Mrisho Kikwete, magazeti yakaibuka na jina la JK. Alipoingia kiongozi wa sasa – Rais Dk. John Pombe Magufuli, jina lake likafupishwa; likawa JPM.

Hakuna chombo kinachoenda kuomba kiongozi aliyeko Ikulu kuridhia jina analopachikwa na vyombo vya habari. Kinachofanywa na magazeti ni ubatizo usiokuwa wa hiari na kubadili jina rasmi kuwa maalum.

Haijawahi kutokea hadharani, ama labda kusikika rais akikataa kuitwa jina analopachikwa na vyombo vya habari. Hii siyo Tanzania pekee, bali maeneo kadhaa duniani.

Majina haya huzoeleka haraka mno na hata mitaani kiongozi husika huanza kufahamika hivyo na kuwa maarufu kuliko hata majina ake rasmi.

Hata hivyo, pamoja na majina haya kukubalika kwa haraka, bado viongozi wengi wanapokuwa madarakani hupachikwa majina mengine zaidi.

Haya majina mengine hutokana na hulka na aina ya uongozi anaokuwa nao madarakani. Pengine hupachikwa majina hutokana na maneno anayopenda kuyarejea kila mara.

Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alipokuwa madarakani na hata sasa, alipachikwa jina la “Mzee Ruksa” hii ilitokana na rais huyo kutamka “Ruksa” akiwa na maana ya kuruhusu mambo mengi kwenda na yasikwamishwe wala kuzingwa na taratibu kwa kiasi kikubwa, almuradi sheria hazivunjwi.

Rais wa Awamu ya Tatu; Benjamin Mkapa, majina yake hayakuwemo katika vyombo vya habari, lakini mitaani na kwenye viunga vya makutano ya watu wengi, alisikika akiitwa “Mzee wa Ukapa.”

Jina la Ukapa, huenda lilitokana na sehemu ya jina lake ubini wake – Mkapa, lakini wengine wakaliweka katika kapu la “hali ya kutokuwa na kitu” – hali mbaya ya uchumi kwa baadhi ya watu, kwamba walikuwa “kapa.”

Mkapa, ndiye kiongozi ambaye hakuwa na majina ya “ubatizo” katika vyombo vya habari, ikilinganishwa na wengine waliomfuatia.

Rais Kikwete, mbali JK, alibebeshwa majina mengine, likiwamo la “Mkwere.” Hili lilitokana na kabila lake – Mkere, watu wa maeneo ya pwani.

Kiasi fulani, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alipachikwa majina mengi. Hayakuwa yakitumika kwenye magazeti, lakini mwenyewe alikiri kuyatambua.

Angalau mawili aliyatamka mwenyewe; Mchonga Meno na Haambiliki. Pamoja na kwamba Mwalimu (sasa marehemu) aliyapinga kwamba yalibeba maana isiyoendana na tabia zake. Hata hivyo, haya yote hayakuwa “rasmi.”

Rais Magufuli, ukiacha ubatizo unaoonekana kuwa rasmi kwa jina la JPM, majina mengine yanayoibukia au yaliyoanza kuibuka mara baada ya kuingia madarakani Novemba 2015, ni pamoja na “Mzee wa Hapa Kazi Tu.”

Jina la au kishangilishi cha – Hapa Kazi Tu; halikushabikiwa sana na magazeti kutokana na urefu wake. Hili haliwezi kukaa vyema kwenye gazeti na pia siyo jepesi kushikika, hata kama linatamkika vyema. Hivyo waandishi ni kama wameliseta. Hawalitumii katika vichwa vya habari kumtambulisha Rais Magufuli.

Vijiweni na kwenye mikusanyiko isiyokuwa rasmi – hasa ya wanachama na wafuasi wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Magufuli anaendeela kutajwa kuwa ‘mzee wa Hapa Kazi Tu.’

Jina hili limetokana na kauli mbiu iliyokuwa ikibeba kampeni za CCM wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ambapo Rais Magufuli alitangazwa na Tumeya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Pamoja na kwamba wengi wamezoea kumuita JPM- jina alilobatizwa na vyombo vya habari, lakini ‘Mzee wa Hapa Hazi Tu’ – bado linabeba maana kutambulisha utendaji kazi wa kiongozi huyo wa Tanzania.

Katika kipindi chake cha miaka inayokaribia mitatu madarakani, Rais Magufuli amethubutu kuchukua hatua na kutenda mengi ambayo watangulizi wake hawakuwahi kuyafanya.

Rais Magufuli siku ya kwanza akihutubia Bunge la Jamhuri na umma, alisema atahakikisha serikali yake inahamia Dodoma na kuweka pembeni hadithi ya kukosekana kwa fedha za uhamisho huo.

Tayari serikali yake imehamia huko, makao makuu halisi ya Tanzania. Ofisi na makazi yake- Ikulu itahamia huko karibuni na kukamilisha uhamisho wa watendaji wa serikali.

Alisisitiza na hatimaye kufanikisha ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo ambalo lina madini ya Tanzanite, Mirerani, Arusha.

Rais Magufuli alisisitiza ujenzi huo akieleza sababu kubwa ni kudhibiti mapato ya serikali katika uchimbaji na biashara ya madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee.

Rais Magufuli ‘alikomalia’ ununuzi wa ndege za abiria na kuzikabidhi kwa shirika la usafiri wa anga nchini (ATCL). Hili aliliweka wazi kwamba, atahakikisha shirika hilo linakufufuka na kukua ili kuwa ‘nembo’ ya Tanzania nje ya nchi.

Hivi sasa Tanzania iko mbioni kuanza mchakato wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji – akiwekeza katika ‘bwawa la stiegler’- mradi ambao umekuwa ukisuasua kusubiri uamuzi wa wakubwa.

Kuanza kwa bwawa hilo la kuzalisha umeme wa maji, ni uthubutu ambao watangulizi wa Rais Magufuli waliukosa wakati wako madarakani.

Kuanza kwa miradi hii mikubwa kunaonesha namna misuli ya kutenda kazi ya Rais Magufuli inavyojengwa na uthubutu mkubwa, hata kama awali ilionekana inaweza kuwa “mzigo” kwa uchumiwa nchi.

Rais Magufuli amekuwa na usemi kwamba – “kama kila kiongozi ataogopa kuanza miradi mikubwa, lini itaanza?”

Ni kutokana na uthubutu wa namna hii, ni vyema jina la – “Mzee wa Hapakazi Tu” likadumu na kubeba utambulisho wa utendaji wa Rais Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

error: Content is protected !!