October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tabia hii ya Ruge ndiyo ilimvutia JPM, Majaliwa

Spread the love

KIFO cha Ruge Mutahaba, aliyekuwa mtayarishaji wa vipindi vya Clouds Media Group (CMG) kimeibua sifa zilizojificha. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Namna Ruge alivyokuwa akifahamika na wananchi ni zaidi ya namna alivyofahamika, kuheshimika na kuchukuliwa na viongozi Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

Moja ya jambo linalobaki kwenye kumbukumbu ya Rais John Magufuli na Kasim Mjaliwa, Waziri Mkuu ni pale Ruge alipotembea nchi nzima kupenyeza mawazo mapya ya kutambua fursa na kuzichangamkia kwa vijana.

Pia alivyokabili mawazo ya vijana na kuwataka kuacha kujenga tabia ya kulalamika na badala yake wachangamkie fursa. Mawazo haya aliyapenyeza mpaka kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu alipokutana nao.

Mambo haya yamemjengea umaarufa mkubwa kwa wananchi na Serikali ya Awamu ya Tano na zaidi, ni pale wakati mwingine alipolazimika kutoa fedha zake kuwawezesha vijana.

“Marehemu alikuwa akitoa hadi fedha zake binafsi kwa ajili ya kuwawezesha vijana hasa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kiuchumi ili nao washiriki katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na hatimaye waondokane na utegemezi,” amesema Waziri Majaliwa.

Haya yote yamebainika baada ya Waziri Majaliwa kutembelea Masaki, jijini Dar es Salaam eneo lililoandaliwa kwa ajili ya msiba wa Ruge aliyefariki juzi tarehe 26 Februari 2019 nchini Afrika Kusini kwa maradhi ya Ini na figo.

Akiwa msibani hapo, Waziri Majaliwa alieleza umma kwamba, Ruge alikuwa ni nyota iliyoangaza kwa vijana wengi.

Kutokana na uimara wake, akili na mwelekeo wake kwa vijana wa taifa hili Waziri Majaliwa amesema, taifa limepoteza nyota wake aliyekuwa akitoa mchango mkubwa kwa vijana huku akilisaidia taifa.

“Ruge kijana aliyekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha vijana wajitambue, wawe wazalendo kwa nchi yao na watambue fursa za maendeleo zilizopo badala ya kuwa walalamikaji,” amesema Majaliwa na kwamba, tabia hii ndiyo iliyoongeza mvuto kwa wananchi na serikali.

Kwa kujua mchango wa Ruge katika nchi hii, muda mfupi baada ya kutangazwa kifo chake, Rais Magufuli alijitokeza hadharani na kuuelezea umma namna alivyoguswa na ‘kijana wake.’

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa ktk tasnia ya habari, burudani, na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema, Amina.” Aliandika Rais Magufuli.

Akiwa msibani hapo Waziri Majaliwa amesema, Ruge ameshirikiana na serikali kuhamasisha vijana kujitambua na kutambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi.

“Hakutaka vijana kulalamikia ajira, alitaka wajitambue na kuchangamkia ajira zinazowazunguka. Hili linampa sifa ya kipekee.”

Amesema, Ruge amefanya kazi ya nchi kwa kusaidia kufungua mawazo ya vijana wengi na kuwaonesha fursa mbalimbali zilizowezesha kuwakwamua kifikra na hatimaye kujitegemea.

Kazi ya Ruge kuinua na kufungua mitazamo na matuamini ya vijana ilianza katika Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

Waziri Kasimu amesema “msiba wa Ruge ni wa wote kwa kuwa alifanya kazi kubwa ya kushirikiana na serikali kuhamasisha vijana kujitambua na kutambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi.

Kazi ya Ruge kwa taifa hili imefahamika si kwa viongozi hao wakuu tu, wanasiasa wengine wameeleza kuguswa na mchango wake wakati alipokuwa uhai.

Umewafungulia Dunia mamia ya Vijana nchini, umekuwa mbunifu na mtambuzi wa fursa mbalimbali, Hakika tumepoteza Shujaa na Mpiganaji mahiri. Pumzika kwa amani Ruge.

error: Content is protected !!