Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Taasisi za dini zaibua dosari uchaguzi 2020, Samia ajibu
Habari Mchanganyiko

Taasisi za dini zaibua dosari uchaguzi 2020, Samia ajibu

Spread the love
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT), imesema taasisi za dini hazikushirikishwa katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020, baada ya kukosa vibali, tofauti na chaguzi zilizopita.Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 8 Julai 2021 na Mwenyekiti wa CCT, Askofu  Alinikisya Cheyo, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano mkuu wa jumuiya hiyo uliofanyika mkoani Morogoro.
Askofu Cheyo ameiomba Serikali ya Rais Samia, izishirikishe taasisi hizo katika michakato ya uchaguzi, kama ilivyokuwa hapo awali.
“Ushirki wa taaisi za dini  katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 haukuwepo kabisa, mara baada ya kukosa kibali katika mamlaka husika. Tunaomba kama tulivyokuwa tunaendelea huko nyuma, tushirikishwe zaidi,” amesema Askofu Cheyo.
Mbali na malalamiko hayo, Askofu Cheyo amesema taasisi hizo zinaomba zishirikishwe katika michakato ya kidemokrasia, hasa kwenye masuala ya utoaji elimu ya uraia na uangalizi wa uchaguzi, kwa wananchi.
“Tunaleta kwako ombi la taasisi za dini kuhusishwa kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia hasa katika  kuwafundisha wananchi  mambo ya uraia na uangalizi wa uchaguzi mbalimbali,” amesema Askofu Cheyo.
Mwenyekiti huyo wa CCT, amesema taasisi za dini zina mchango mkubwa katika masuala ya utungwaji na marekebisho ya  sheria, hivyo zinapaswa kushirikishwa.
“Pendelezo letu la kwanza, ni nafasi ya taasisi za kidini kuhusishwa katika michakato ya kidemokrasia, taasisi zimekuwa zikishiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia,  kutokana na ukaribu na muundo wake,” amesema Askofu Cheyo na kuongeza:
“Ikiwa pamoja  na kutoa maoni katika utungwaji na maboresho ya sheria, kutoa elimu ya uraia na kushiriki uchaguzi.”
Akijibu ombi la taasisi hizo kushirikishwa katika michakato ya uchaguzi, Rais Samia amesema Serikali yake itafuatilia masuala ya kisheria,  ili kuona namna taasisi hizo zinashiriki.
 “Kuna taasisi zinashiriki mambo ya uchaguzi zilizosajiliwa chini ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ( NGO’s), nadhani hapa kuna utata wa kisheria hizi zimesajiliwa huku na zingine kule.  Kwa maombi yenu haya inabidi tuangalie sheria zetu zinasemaje,  ili kuwapa uhalali wa kufanya shughuli hizo,” amesema Rais Samia.
Kuhusu taasisi hizo kushiriki katika utungwaji na maboresho ya sheria, Rais Samia amesema kabla ya Bunge kupitisha sheria,  hutoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni yao kuhusu mchakato husika, hivyo amezitaka zitumie nafasi hiyo.
“Niseme kwamba katika kutoa maoni kwenye maboresho na utungaji Sheria, Bunge limetoa siku maalumu kutoa maoni kwa wananchi. Siku hii taasisi zinaweza kushiriki kutoa maoni yao.  Hili la kushirikishwa kutoa elimu ya uraia nalo ni zuri sana, tutawashirikisha,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia amesema Serikali zilizopita zilikuwa zinashirikisha taasisi za dini,  katika masuala ya kidemokrasia na kukumbushia namna viongozi wa dini walivyoshiriki katika Bunge la Katiba.
“Serikali zilizopita zimekuwa zikifanya hivyo, kushirikisha viongozi ikiwemo katika masuala ya kidemokrasia. Nakumbuka nilipokuwa makamu mwenyekiti wa  Bunge la Katiba,  sura za baadhi ya viongozi wa dini niliziona,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“ Huku ni kushirikishwa katika mambo ya kidemokrasia , nitafuata nyayo za walionitangulia kufuata hili.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Kasilda Mgeni anasisitiza umoja, ushirikiano Same 

Spread the love  MKUU mpya wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

Habari MchanganyikoTangulizi

Breaking news! Mufti amng’oa Sheikh mkoa Dar

Spread the loveBARAZA la Ulamaa la Bakwata katika kikao kilichofanyika tarehe 1...

Habari Mchanganyiko

Bilioni 120 za DMDP zaibadilisha Ilala, wananchi watoa ya moyoni

Spread the loveJUMLA ya Sh bilioni 120.7 zimetumiwa na Halmshauri ya Jiji...

error: Content is protected !!