WAKATI Soka la wasichana likichipua kwa kasi Taasisi ya Karibu Tanzania Organization ‘KTO’ na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imezidi kuchagiza ukuaji wa soka kwa kutamatisha mafunzo ya makocha wa kike 54. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Makocha hao waliopikwa kwa muda wa wiki mbili chini ya usimamizi wa TFF wametoka kwenye Vyuo vya maendeleo ya Wananchi (FDC’s) kupitia mpango wa mpira fursa.
Hayo yamethibitika mwisho wa wiki iliyopita terehe 3 Machi 2023, wakati wa ghafla ya kuwakabidhi vyeti makocha 54 waliohitimu mafunzo ya awali ya ukocha.
Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF, Hawa Mniga amesema kitendo cha KTO ni wazi kuwa imeunga mkono jitihada za serikali katika kuliinua soka la wanawake nchini.
Amesema kuwa na idadi kubwa ya makocha wa kike kutongeza wachezaji mahili nchini na kutaifanya nchi yetu kuwa bora zaidi kwenye upande wa soka la wanawake.
“Tunaamini kuongezeka kwa walimu kutafanya tuwe na wachezaji wengi wazuri na soka letu litakua zaidi” alisema Mninga.
Amesema, kupitia programu ya Mpira Fursa inayotekelezwa na KTO lengo la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la kufundisha Mpira na kutoa wachezaji bora wa soka, waamuzi na walimu wa mpira wa miguu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na Shirika hilo kutoa mafunzo ya ukocha na kuongeza idadi ya makocha wanawake wanaotambuliwa na TFF kwa jitihada za KTO.
Mniga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kutumia maarifa hayo kwa bidii ili kuweza kutoa matunda bora katika soka la wanawake Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (TVET) Margareth Massai amesema, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) inatambua jitihada za KTO hasa kupitia programu ya mpira fursa ambayo imewapa kitu cha ziada wanafunzi.
“Katika kutekeleza programu ya Elimu Haina Mwisho tukaona ombwe katika utekelezaji , KTO wakaja na wazo hili la Mpira Fursa ambalo limeleta matokeo chanya kwa kuwachangamsha, kujiamini na kuondoa mawazo potofu kwamba Wasichana hawawezi.” Amesema.
Naye Mkurugenzi wa KTO, Maggid Mjengwa amesema kuwa Taasisi hiyo inatekeleza kwa vitendo falsafa ya ‘Mpira uchezwe kila Kona na kila Mtaa’ na kwenda sambamba na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amelipa jicho la pekee sekta hiyo ambayo imeanza kuonesha matumaini makubwa baada ya baadhi timu kushiriki mashindano kwa ngazi mbalimbali za kimataifa.
Mjengwa alisema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa michezo katika kuhakikisha mpango mkakati wa ushiriki wa Taifa katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo ya kombe la dunia 2030 unafikiwa kwa mafanikio makubwa na hiyo ni pamoja na kuendelea kunoa vipaji kuanzia ngazi ya chini.
Akieleza kuhusu programu ya Mpira Fursa Mkurugenzi wa programu wa KTO Mia Mjengwa alisema programu hiyo imelenga kuendeleza soka la wanawake na Wasichana nchini na ilianzishwa na KTO kwa kushirikiana na TFF na inaendeshwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) vilivyopo kote nchini.
Amesema, mafunzo hayo kwa makocha wa ngazi ya chini kutoka vyuo hivyo kwa wiki mbili chini ya wakufunzi wa TFF itasaidia kufikia timu zipatazo 216 za soka za Wasichana ambazo zitaanzishwa katika shule za Msingi 54 katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54.
Leave a comment