January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Taasisi ya Nyerere yabeba dhamana ya amani

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku (katikati) akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni Gallus Abedi, Msaidizi wa Mkurungezi wa taasisi hiyo na Edgar Atubene, Afisa Mipango.

Spread the love

HALI tete ya dalili za uwepo wa viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani, vimeishtua Taasisi ya Mwalimu Nyerere na hivyo kuchukua jukumu la kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wakuu wa vyama ili kuleta utengamano. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mkutano huo utajadili amani, umoja na utulivu wa nchini. Utafanyika 19 – 20 Mei mwaka huu, kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, Joseph Butiku – Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, amesema “tunawakutanisha viongozi hao kwa kuzingatia kuwa wao ndio wenye jukumu na wajibu wa kwanza wa kusimamia amani na umoja na kuhakikisha misingi yake inaimarishwa na kudumishwa”.

Ameyataja majukumu mengine waliyonayo viongozi hao kuwa ni kusimamia kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

“Majukumu haya yanahitaji kuaminiana, miongoni mwa Watanzania hasa kuaminiana miongoni mwa viongozi wote na kuzingatia misingi muhimu ya ukweli, uwazi, heshima ya utu, uhakika na matumaini ya maisha bora,” amesema.

Akinukuu hotuba ya hayati Julius Nyerere aliyoitoa mjini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Taifa wa Tatu wa CCM, Oktoba 22, 1987- Butiku amesema “panapokuwa hapana haki wala amani na matumaini ya haki, hapawezi kuwa na amani na utulivu wa kisiasa. Hatma yake patazuka fujo, utengano na mapambano.”

“Baadhi ya viashiria vya kukosekana kwa amani nchini ni matumizi ya nguvu kubwa kupita kiasi yanayofanywa na vyombo vya dola, matumizi mabaya na ubadhirifu wa rasilimali za taifa kama vile madini na gesi, ardhi, wanyama pori,  suala la Muungano katika Katiba mpya, rushwa na uvunjifu wa katiba za vyama na katiba ya taifa,” amesema.

Butiku amesema “Taasisi ya Mwalimu Nyerere inajua kuwa suala la Muungano halijaisha. Bado kuna ubishi kuhusu suala hili. Ubishi huu sio vizuri ukafunikwa funikwa. Utahatarisha amani ya nchi.”

Amevitaja viashiria vingine kuwa ni migogoro ya kidini inayojidhihirisha kati ya Wakristo na Waislam hasa kuhusu Mahakama ya Kadhi; rushwa iliyokithiri, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wazee na vikongwe na uvamizi wa vituo vya polisi.

Vingine ni kuua polisi na kupora silaha kwenye vituo vya polisi, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafuagaji, migogoro ya ardhi kati ya wanavijiji na wawekezaji na wachimbaji wa madini wakubwa na wadogo.

Aidha, Butiku amesema hoja hiyo itawasilishwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere huku viongozi 14 wakichangia maoni katika ripoti yenye kurasa 62 ambayo kesho itawasilishwa kwenye mkutano.

Baadhi ya viongozi hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

error: Content is protected !!