Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Taasisi ya Mwalimu Nyerere yapewa zigo kuponya Taifa, wanasiasa watoa nyongo
Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Taasisi ya Mwalimu Nyerere yapewa zigo kuponya Taifa, wanasiasa watoa nyongo

Julius Nyerere, Hayati Baba wa Taifa
Spread the love

 

TAASISI ya Mwalimu Nyerere (MNF) nchini Tanzania, imeombwa kuandaa kikao cha mariadhiano ambacho kitawakutananisha viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini ili waweze kuponya taifa. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa na viongozi mbalimbali wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu ambao walishiriki mdahalo wa kitaifa kuhusu kushirikiana ili kudumisha na kuimarisha udugu, uzalendo, uwajibikaji, amani, maridhiano na maendeleo uliondaliwa na taasisi hiyo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Katibu wa Baraza la Wazee Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Roderick Lutembeka, alisema ili taifa liweze kuponywa ni vema kukawepo vikoa vya maridhiano vitakavyo shirikisha viongozi wakuu wa vyama.

Lutembeka alisema katika kipindi cha miaka mitano, Watanzania wameshuhudia wapendwa wao wakipotezwa katika mazingira yakutatanisha hivyo wakati umefika MNF kutumia nafasi yake kumuomba kiongozi wa nchi kuunda tume huru ambayo itaongoza maridhiano hayo.

“Mimi ni miongoni mwa Watanzania ambao wanaonya yanayoendelea na ninasisitiza kuwepo maridhiano kwani ndio njia sahihi ya kulinusuru taifa.”

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

Nitumie nafasi hii kuiomba Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuchukua ombi hilo na kuangalia namna ya kulifikisha kwa mamlaka husika ili kunusuru nchi,” alisema.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu alisema chama chao kinaamini katika maridhiano ila akasisitiza hilo linaweza kufanikiwa iwapo wanaotaka maridhiano wana nia ya dhati.

Semu alisema asilimia kubwa ya jamii imejawa na unafiki na ubinafsi hali ambayo inakwamisha mikakati yote ya kuhakikisha jamii inakuwa moja kwenye masuala ya kitaifa.

“Sisi tupo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, tunapitia mazingira magumu lakini dhamira yetu ni kuangalia maslahi mapana ya Wanzazibar ndio maana hadi sasa tupo,” alisema.

Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Bara

Naye Kada wa chama hicho Kudra Garula alisema, kuongezeka kwa chuki ndani ya jamii kunachangiwa na baadhi ya watu kujiona wao ndio wenye haki ya kutawala katika nchi jambo ambalo halikubaliki.

“Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha Tujisahihishe amezungumzia unafki, ubinafsi, uongo na mengine mengi na akasisitiza tatizo kubwa la Watanzania ni ubinafsi ambapo wapo wanaotaka wapate wao tu hali ambayo inaitafuta Tanzania kwa sasa,” alisema.

Garula alisema Nyerere alithubutu kukemea maovu lakini kwa sasa hakuna kiongozi yoyote ambaye anaweza kuthubutu kufanya hivyo kwa sababu wamejawa na unafki, ubinafsi na uongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma ya Chama cha NCCR-Mageuzi,  Edward Simbeye alisema, alisema siku zinavyoendelea vijana wanaendelea kukataa tamaa jambo ambalo halina afya kwa nchi.

Edward Sembeye, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR Mageuzi

“Naomba wazee wetu nyie msikubali kuondoka mkaacha taifa limegawanyika vipande kisa madaraka, sisi NCCR –Mageuzi tumekuwa tukisisitiza maridhiano tukiamini ni njia sahihi ya kufikia muafaka pale ambapo kuna mgogoro baina yetu,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Pambalu aliitaka Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuishi katika maeneo ya mwasisi wake Hayati Nyerere kwa kukemea watawala pale ambapo wanakosea bila kupepesa macho.

Pambalu alisema viongozi wa vyama vya siasa wanapitia wakati mgumu katika kufanya siasa nchini hivyo ni vema MNF kukemea hali hiyo ili haki, amani na udugu viweze kutendeka.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Steven Wassira alivitaka vyama vya upinzani kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa kero na madukuduku yao.

“Ni kweli miaka ya hivi karibuni kulikuwa na changamoto lakini sasa tuna kitabu kipya ambacho kina miezi saba tu madarakani ni vigumu kufanya mambo yote kwa pamoja tumpe ushirikiano muafaka utapatikana,” alisema.

Naye Mjumbe wa Halamashauri Kuu ya CCM, Jafari Kubecha alishauri vyama vya upinzani kutumia fursa ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa ambalo lipo chini ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutatua changamoto wanazokutana nayo.

Steven Wasira

Kubecha alisema yaliyotokea kipindi cha nyuma yanapaswa kufukiwa na kusahaulika kwa kuwa hayawezi kubadilika kwa sasa.

Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa Chama cha ADC, Hassan Mvungi alisema mdahalo huo uliondaliwa na MNF, ni vema ukawa endelevu  ili kuhakikisha wanasiasa wanapata nafasi ya kuzungumza madhila wanayopitia, huku akisisitiza maadili na uzalendo vipewe kipaumbele.

Naibu Katibu Mkuu  wa Chama cha NRA, Rachel Balama alitoa wito kwa wanasiasa na wafuasi wao kujikita katika misingi ya utaifa kabla ya kuchukua hatua zozote ili nchi iwe salama.

Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alisema pamoja na mambo mengine ambayo wanapitia jambo la msingi ni uvumilivu baina yao kwa maslahi ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mtoa mada Dk. Beatrice Mkunde, kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alisema katika kuhakikisha dhana ya demokrasia, haki, uhudu na udugu vinatendeka ni lazima kuwepo na Katiba nzuri inayotokana na wananchi.

Alisema iwapo wananchi wataridhia mchakato huwa viema wakazingatia uadilifu na kuepuka  kuhodhiwa na wanasiasa na makundi yenye maslahi yanayotafuta kuongoza taasisi za kisiasa kwa manufaa yao wenyewe.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Rodrick Lutembeka

“Mfano sharia za kinga dhidi ya baadhi ya viongozi; kinga dhidi ya baadhi ya taasisi kutokaguliwa. Hivyo basi, bila katiba imara inayozingatia matakwa halisi ya wananchi na siyo matakwa binafsi ya watawala, demokrasia halisi itaishia kuwa ni maneno ya propaganda huku haki za wananchi zikiendelea kukanyagwa,” alisema.

Naye Msaidizi Maalum wa Mkurugenzi wa MNF, Gallus Abedi alisema taasisi hiyo inaamini katika majadiliano jambo ambalo limeweza kurejesha amani katika maeneo mbalimbali duniani.

Abedi alisema pamoja na kuamini katika maridhiano ni vema wenye mamlaka wakasimamia haki, usawa na uhuru kama nguzo muhimu ya kutekeleza majukumu yao.

Awali, akifungua mdahalo huo, Mkurugenzi wa MNF, Joseph Butiku alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la (IRI), wamedhamiria kutoa nafasi ya kujadiliana na wadau katika eneo la kudumisha na kuimarisha udugu, uzalendo, uwajibikaji, amani, maridhiano na maendeleo kwa kuwa ni muhimu kwa ustawi wa nchi.

Butiku alisema, MNF inaamini katika majadiliano hivyo wataendelea kuandaa midahalo ya aina hiyo kila mara ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa kitu kimoja.

“Hayati Mwalimu Nyerere aliamini katika midahalo na sisi kila tukipata fedha za kuwakutanisha wadau wa kisiasa na asasi za kiraia tutafanya hivyo kwa maslahi ya nchi na wananchi. Tutakuwa wa mwisho kuona watu wanafarakana kwenye mambo ambayo yanazungumzika,” alisema.

Naye Ofisa Program Mwandamizi wa IRI, Lulinga Asaph alisema shirika hilo lina amanini katika majadiliano na mazungumzo katika kufikia muafaka hivyo wataendelea kushirikiana na MNF katika kampeni hiyo ya kujenga umoja na ushirikiano.

Lulinga alisema IRI inaamini vyama vya siasa ni mdau mkubwa katika kulinda amani, umoja, haki na upendo nchini hivyo vinapaswa kutumia midahalo hiyo kuleta matumaini kwa wafuasi wao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!