Wednesday , 24 April 2024
Home Kitengo Habari Taarifa kuhusu mwaka mmoja wa kufungiwa MwanaHALISI
HabariTangulizi

Taarifa kuhusu mwaka mmoja wa kufungiwa MwanaHALISI

Gazeti la MwanaHALISI
Spread the love

NI mwaka mmoja kamili leo (30 Julai 2013) tangu serikali ifungie gazeti la MwanaHALISI. Kifungo kinaendelea chini ya amri ya kuzuia uhapishaji “kwa muda usiojulikana.” Zimekuwa siku 365 za kulia na kusaga meno.

Ndani ya kipindi hiki wasomaji wetu wamesubiri, kusubiri na kusubiri, lakini serikali imekaa kimya. Imeendelea kung’ang’ania kauli yake ya 30 Julai 2012, kupitia Msajili wa Magazeti (MAELEZO) kwamba tumezuiwa kutoa gazeti na kwamba tusome amri hiyo katika Toleo Na. 258 la Gazeti la Serikali.

Katika kipindi hiki, waandishi wa habari wa MwanaHALISI wamekuwa wahemeaji wa vibarua katika vyombo mbalimbali vya habari ili waweze kuishi. Familia zao zimejaa ukame wa chakula, kitoweo na maji ya kunywa. Ndugu zao waliowategemea wamekuwa miongoni mwa wapiga miayo mchana na usiku. Baadhi ya watoto wa familia hizi wanakosa nauli ya kwenda shule. Serikali imekaa kimya.

Ni ndani ya kipindi hiki, wafanyakazi wa idara nyingine za MwanaHALISI wamekumbwa na msononeko na baadhi kupata msongo wa mawazo. Wauza magazeti wamepigwa na ukame usiomithilika, kwani gazeti waliloweka mbele na lililokwenda kasi, lilizimwa na serikali yao.

Umekuwa mwaka mmoja wa kukosa mapato ya kila wiki kwa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited ambayo ndiyo mchapishaji. Tumekuwa tukipata tu salaam za wanaotutakia mema; kauli za kulaani serikali; vilio vya waliokosa taarifa na habari za kina na zenye kuchochea wahusika kuchukua hatua. Tumekuwa tukipokea sala kuombea waandishi na wafanyakazi wengine wasio na ajira; na sala za kuombea serikali ya Rais Kikwete kufunguka na kutambua umuhimu, haki na uhuru wa jamii kupata taarifa kutoka gazeti lao.

Kampuni yetu ya uchapaji imefanya juhudi kubwa za kutaka gazeti lake lifunguliwe. Miongoni mwa jitihada hizo ni kumwandikia rais. Hatukujibiwa.

Tarehe 13 Agosti 2012, tulitoa taarifa kwa Msajili wa Magazeti tukieleza dhamira yetu ya kubadilisha gazeti la MSETO – maalum kwa habari za michezo na burudani – kuwa la habari za mchanganyiko, zikiwemo za siasa, uchumi na jamii.

Siku moja baada ya kutoa taarifa ya kubadilishwa kwa gazeti la MSETO, serikali ilitutaka kutekeleza mambo saba. Tulifanya hivyo siku ya pili. Leo ni siku ya 346 tangu kutoa taarifa ya kutaka kubadilisha gazeti hilo. Serikali imekaa kimya.

Tulipotaarifu msajili wa magazeti kuwa sasa tunaanza kutoa gazeti la MSETO kama Bodi ya Wakurugenzi ilivyoamua, msajili akasema gazeti lisifanye mabadiliko hadi “Menejementi ya Hali Halisi Publishers Ltd., itakapokutana na waziri mwenye dhamana ya habari katika tarehe itakayopangwa mapema Januari 2013.” Hiyo ilikuwa 24 Desemba 2012.

Januari imekuja na kwenda. Februari, Machi, Aprili, Mei, Juni, sasa Julai – miezi saba – lakini hakuna dalili zozote za kuitwa kukutana na waziri. Hapa katikati tumekumbusha mara mbili. Serikali haijajibu.

Watu binafsi, asasi za kijamii, nchi mbalimbali wahisani, wakiwamo mabalozi wa Jumuiya ya Ulaya, wametoa matamko na wito kwa serikali kufungulia gazeti la MwanaHALISI. Serikali imekaa kimya.

Kilio cha wote hawa kinatokana na kuthaminika kwa kazi iliyofanywa na gazeti letu kwa miaka saba hadi likawa chombo halisi cha umma. Hata likiwa kifungoni, kwa mwaka mzima huu wa nane, gazeti limeendelea kuwa kwenye midomo ya wengi katika mijadala, maandishi na mawasiliano ya ujumbe wa simu za mikononi. Hii ina maana pia kuwa gazeti liko mioyoni mwa wengi.

Bado tunaona serikali ina nafasi ya kulifungulia gazeti hili. Kwanini? Kwa kuwa hakukuwa na sababau yoyote ya kulifungia – kimaandili na kitaaluma. Hili tuliishalieleza katika barua yetu kwa rais.

Tunasubiri serikali ifungulie MwanaHALISI. Tunaisihi isikilize kilio cha wote wanaopaza sauti za kudai haki na uhuru wa habari na uhuru wa kuandika habari. Inawezekana ikasikia leo. Tuendelee kuiambia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

error: Content is protected !!