June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Taa ya habari haipaswi kuzimika

Waandishi wa habari wakiwa kazini

Spread the love

TASNIA ya habari ni taa ya umma inayomulika na kuangaza kwenye giza na kuonyesha wazi yaliyojiri humo pamoja na kufichua maovu kwa faida na maslahi ya umma.

Taa hii muhimu haipaswi kuzimika, japo zipo mbinu chafu za baadhi wasioitakia mema taa hii na hivyo kufanya kila hira ili kuizima. Juhudi hizo ni pamoja na kuififisha kwa rushwa.

Baadhi ya wanahabari wanatumia kisingizio cha maslahi duni kama kigezo cha kuomba rushwa ili kuzima masuala nyeti katika jamii.

Taa hii ikizimwa taifa litakua kwenye giza la rushwa na maovu kwa sababu hakuna wa kuyamulika na kuyakemea tena. Kwa bahati mbaya taa hii inapendwa na watu wachache wapenda haki ila kwa waovu wanaiona kama inawazibia njia.

Wanahabari wamefanikiwa kufichua mambo yanayolitafuna taifa hili na hivyo kudhoofisha uchumi wake kukua ukimlenga mwananchi wa kawaida. Hata hivyo kazi hiyo nzuri bado inadhoofishwa kwa vikwazo mbalimbali.

Kuna usemi kwamba, “Huwezi kula vidole vinavyokulisha”. Kumbe kama watenda maovu wataendelea kuwalisha na kuwanywesha wanahabari, ukweli utakuwa umeuawa. 

Ukweli siku zote unauma, waandishi wanaokula rushwa hawataweza kuwauma wala rushwa wenzao kwa sababu na wao wamepata mgao.

Hivi ndivyo tasnia ya habari inavyoenda kuzimika kama kibatari katikati ya upepo mkali wa rushwa, vitisho, mauaji ya waandishi, kutekwa na kujeruhiwa vibaya. 

Sote tunakumbuka yaliyomkuta ndugu yetu hayati Daudi Mwangosi, aliyeuawa kikatili katika mikono ya polisi, Absalom Kibanda, alivyokamatwa na kuteswa vibaya hadi kutobolewa jicho lake. Tunamkumbuka pia Saed Kubenea alivyomwagiwa tindikali machoni na Ndimara Tegambwage alivyokatwa mapanga.

Yote haya yanadhihirisha kuwa kazi ya uandishi wa habari haimfurahishi kila mtu. Wanaosema ukweli wanawindwa na wanaosema uongo wanalindwa.

Mambo haya yanafanywa na wasiopenda mwanga wa tasnia. Wanapenda giza maovu yao yasimulikwe kamwe, wako tayari kuyafunika kwa gharama yoyote hata ikibidi kumwaga damu za watu.

Mwandishi wa makala haya ni Ferdinand Shayo, anayepatikana kwa barua pepe; ferdinandshayo@gmail.com na simu; 0765938008

error: Content is protected !!