Sunday , 19 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Sura halisi ya Mwakyembe sasa inaonekana
Habari Mchanganyiko

Sura halisi ya Mwakyembe sasa inaonekana

DK. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Spread the love

Na Saed Kubenea

DK. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametoa amri ya kuzuia uchapishaji wa gazeti la Tanzania Daima, kwa muda wa siku 90 kuanzia leo, Jumanne, 24 Oktoba 2017.

Kifungo dhidi ya Tanzania Daima kimefuatia madai kuwa gazeti limeripoti kimakosa takwimu za watu wanaotumia ARV (madawa ya kulefusha maisha).

Kwamba badala ya gazeti kuripoti kuwa asilimia 67 ya walioathirika wanatumia ARV, lenyewe limeandika, asilimia 67 ya Watanzania wanatumia madawa hayo. Hilo ndilo kosa la gazeti hili linalochapishwa kila siku.

Tanzania Daima linakuwa gazeti la tano kufungiwa ndani ya kipindi cha miaka miwili cha utawala wa John Pombe Magufuli. Magazeti mengine yaliyofungiwa ni pamoja na MwanaHALISI, MAWIO, MSETO na Raia Mwema.

Magazeti ya MwanaHALISI na MAWIO yamefungiwa kwa muda wa miaka miwili; MSETO limefungiwa kwa mwaka miaka mitatu na Raia Mwema limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu. Binafsi naliangalia tukio hilo kwa macho matatu:

Kwanza, huu ni muendelezo wa mtawala mkuu wa nchi kuwatumia watu wasiojiamini, wanaopenda kujipendekeza na wenye sura mbili, kutimiza kile anachokitaka.

Yupo katika wizara hiyo kwa kazi maalum ya kumtumikia “bosi wake.”

Pili, kufungia gazeti kwa kosa la “kuteleza ulimi,” kunazidi kuashiria kuwa hapa tulipofika – siyo tuendako – ni pabaya mno. Gazeti siyo msahafu. Linaendeshwa na binadamu na hivyo linaweza kukosea.

Hatuwezi kuendesha magazeti, radio au televisheni kwa kuviziana. Hatuwezi kuendesha vyombo vya habari kwa kuangalia nani mmiliki na nani mhariri. Haiwezekani.

Mifano ya magazeti na vituo vya televisheni kukosea ni mingi. Mfano, televisheni ya serikali (TBC), iliwahi kutangaza taarifa za uwongo tena wa makusudi, kuwa rais wa Marekani amemsifia Rais wa Tanzania, John Magufuli, lakini haijawahi kuchukuliwa hatua.

Tatu, kufungia gazeti hili, kumewafanya waandishi wa habari wa magazeti yetu kupoteza “matumaini” machache yaliyosalia ya kuwa “wahemeaji wa vibarua katika vyombo vingine vya habari.

Ndugu zao waliowategemea wameungana nao katika kupiga miayo mchana na usiku. Hii ina maana kuwa baadhi ya watoto wa familia hizi watakosa nauli ya kwenda shule. Serikali itakosa mapato na wananchi maelfu watakosa ajira.

Ndani ya HHPL – wachapishaji wa MwanaHALISI, MAWIO na MSETO, tumekuwa tukipata tu salaam za wanaotutakia mema; kauli za kulaani serikali; vilio vya waliokosa taarifa na habari za kina na zenye kuchochea wahusika kuchukua hatua.

Tumekuwa tukipokea sala za kuombea waandishi na wafanyakazi wengine wasio na ajira; na sala za kuombea serikali ya Rais Magufuli ya kutambua umuhimu, haki na uhuru wa jamii kupata taarifa kutoka magazeti yao.

Ni ndani ya kipindi hiki, wafanyakazi wetu wa idara nyingine wamekumbwa na msononeko na baadhi kupata msongo wa mawazo.

Ni rai yangu kuwa kila aliyefungiwa gazeti lake kukimbilia mahakamani kupinga “ukoloni huu.” Sisi tuko tayari mahakamani kwa kuwa tunaamini hakukuwa na sababau yoyote ya kulifungia “kimaandili na kitaaluma.”

Jambo ambalo baadhi yetu hatulifahamu ni wapi serikali inakopata kiburi cha kufungia magazeti. Kwa nini haitaki kusikiliza kilio cha watu binafsi, asasi za kijamii, nchi mbalimbali wahisani, wakiwamo mabalozi wa Jumuiya ya Ulaya, wanaotoa matamko na wito kwa serikali kufungulia magazeti haya?

Kwa mfano, wananchi na wahisani wamekuwa wakililia MwanaHALISI. Kilio cha wote hawa kinatokana na kuthaminika kwa kazi iliyofanywa na gazeti letu kwa miaka 10 hadi likawa chombo halisi cha umma.

Hata lilipokuwa kifungoni kwa muda wa miaka mitatu – Julai mwaka 2012 hadi Septemba mwaka 2015 – gazeti limeendelea kuwa kwenye midomo ya wengi katika mijadala, maandishi na mawasiliano ya ujumbe wa simu za mikononi. Hii ina maana pia kuwa gazeti liko mioyoni mwa wengi.

Bado tunaona serikali ina nafasi ya kulifungulia gazeti hili. Kwanini? Tunasubiri serikali ifungulie MwanaHALISI. Tunaisihi isikilize kilio cha wote wanaopaza sauti za kudai haki na uhuru wa habari na uhuru wa kuandika habari. Inawezekana ikasikia leo. Tuendelee kuiambia.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Canada yatenga bilioni 38 kutekeleza mradi ya kuinua vijana TZ

Spread the loveSERIKALI ya Canada kupitia ‘CARE International Canada’ imetenga takribani Sh...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari Mchanganyiko

Balile ateuliwa rais wa wahariri Afrika Mashariki

Spread the loveJumuiya ya Wahariri wa Afrika Mashariki (EAES), imemchagua Mwenyekiti wa...

error: Content is protected !!