January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sumaye: Nitaboresha uchumi kwanza

Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye akitangaza nia ya kuwania Urais leo jijini Dar es Salaam

Spread the love

WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Tluway Sumaye (65), amesema walioatanagaza nia ya kugombea urais ndani ya CCM, hawawezi kuboresha elimua kama kipaumbele namba moja bila kuboresha uchumi wa nchi kwanza. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Sumaye ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza nia ya kuwaomba uteuzi wa chama chake katika mkutano wake wa ndani aliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wafuasi wake.

Sumaye ambaye amekuwa waziri mkuu kwa miaka 10 mfululizo katika serikari ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa amesema, “huwezi kuzungumzia kuboresha elimu, afya, amani kama huna fedha. Lazima kwanza uanze kwenye uchumi”.

“Kama nitapewa ridhaa ya kuiongoza nchi hii kipaumbele changu namba moja ni kuimarisha uchumi hasa katika maeneo yanayohusisha watu wengi. Hili nitalifanikisha kwa kuendeleza kilimo na kuimarisha masoko kwa kulinda viwanda vya ndani,” amesema Sumaye.

Sumaye amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni kulinda muungano, amani na utulivu; kupambana na maovu ikiwemo rushwa, ufisadi, madawa ya kulevya na mauaji; kuboresha huduma za jamii; kuongeza ajira na kuimarisha michezo na utamaduni.

“Nikiingia madarakani nitaunda vyombo vya kuchunguza rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi. Kisha nitaunda Mahakama Maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala haya. Sitaungana na wala rushwa, nitatoka ndani ya CCM kama CCM watapitisha mla rushwa na siamini kama chama kitachagua mla rushwa,” amesema Sumaye.

Kuhusu sifa za mtu anayaefaa kuwa Rais, Sumaye amezitaja kuwa ni “ kwanza, awe tayari kujipima, kujitafakari na ajiridhishe anatosha kiafya, kiakili, kimaadili na kidhamira. Pili awe tayari umma umpime na siyo ajipime mwenyewe”.

Akizungumzia kuhusu matarajio ya Watanzania kuhusu Rais wanayemtaka, Sumaye amesema lazima awe mtumishi wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, mzalendo wa dhati, mwaminifu na mwadilifu, jasiri na mtiifu wa katiba na sheria.

“Sifa nyingine ni awe anafikiri na anashaurika, atayeweka serikali itakayowajibika kwa umma, atalinda maslahi ya umma, atalinda amani na muungano, awe na uwezo wa kusimamia uchumi, atakayeziba pengo la walionacho na wasionacho na atakayeboresha huduma za jamii,” ameeleza Sumaye.

Aidha, Sumaye ameyataja mafanikio yaliyofikiwa na serikali aliyoisimamia akiwa Waziri Mkuu kati ya mwaka 1995 – 2005 kuwa ni kukuza uchumi ambapo mfumko wa bei ulikuwa zaidi ya asilimia 27 ambapo walifanikiwa kuushusha hadi asilimia nne.

 

“Awamu ya tatu tulipambana na rushwa. Miaka yote 10 mkate, nyama, sukari havikupanda bei hovyo. Tulikuta madeni mengi sana ndani na nje ya nchi. Nchi yetu ilikuwa kati ya nchi nne masikini duniani. Tukasamehewa madeni lakini ni baada kudhibiti hali ya uchumi,” amesema Sumaye.

Ameyataja mafanikio mengine ambayo yalitokana na uongozi wake ni; kulibomoa jiji la Dar es Slaam na kuliweka katika hali ya usafi, kuanzia Televisheni ya Taifa, kuanzisha na utekelezaji wa miradi  Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).

Akizungumzia kuhusu kuhusika katika kashfa ya ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma na uuzaji wa nyumba za serikali kwa bei ya kutupwa, Sumaye amesema “Sera ya ubinafsishaji ilikuwepo kabla ya Rais Mkapa. Ilipitishwa bungeni na vikao vyote vya maamuzi. Hivyo kuna ubaya gani mimi kuitekeleza”.

Aidha, Sumaye amesema katika uongozi wake hatasahau ajali ya Mv Bukoba, ukame wa mwaka 1978 uliosababisha baadhi ya balozi kuanza kuondoa watumishi wake nchini, mvua za El- Nino za mwaka 1998 na kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo kwa siku tatu mfululizo hakulala kwa ajili ya kuhakikisha serikali inafanikisha kuendesha msiba huo.

Maswali

Swali 1: Katika awamu uliyoongoza ziliibuka kashifa kama Meremeta, uuzwaji wa benki ya NBC, Rada na uuzwaji wa mgodi wa Kiwira haya yalikushindaje?

Jibu: Kuhusu kashfa zilizojitokeza, kwanza niseme ni kweli mimi nilikuwa mshauri wa Rais. kuna vitu vimeitwa kashfa lakini mimi sioni kama kashfa mfano uuzwaji wa benki ya NBC si kashfa, hii benki haikua ikitoa kodi yoyote hazina, gavana wa benki alitoa tahadhari kuwa kwa madeni ya NBC ukipanga noti za elfu kumi zinazidi urefu wa mlima Kilimanjaro.

Ubinafsishwaji wake ulitangazwa lakini pia haikuuzwa yote na ndio iliyozaa NMB ya leo. Hakuna mwehu aliyekaa na mwenzake wakauzina NBC hotelini. Hakuna.Zingine zote zinafanana. Rada, ndege ya Rais na mengineyo.

Swali 2: Eleza mali unazomiliki ili Watanzania wajue na pia tuambie nani anakupa homa miongoni mwa wagombea unaogombea nao?.

Jibu: Watanzania wananijua, watoto wangu mnawajua wanafanya kazi za kawaida za serikali. Mchungaji Christopher Mtikila alinituhumu mambo mengi sana, baadaye akasema watu wasafi nchi hii ni Sumaye, Jaji Joseph Warioba na Dk. Harrison Mwakyembe. Hela nyingine ambayo nilipata nilisomesha waandishi wa habari nyie mnajua. Mimi nina ‘moral authority’ kwa muda mrefu. Kwa waliojitokeza sasa hivi hakuna hata mmoja ambaye ni tishio kwangu.

Swali 3: Tumekwama kwenye mchakato wa Katiba, unawaahidi nini wananchi ambao maoni yao yalitupwa na Bunge Maalum la Katiba?

Jibu: Kuhusu Katiba mpya. Tangu mchakato unaanza nilisema usimamizi ni muhimu kuliko hata katiba kwa sababu hata ikiwa nzuri wasipokuwepo wasimamizi wazuri mambo yatakwenda hovyo.

Swali 4:  Ukiwa Waziri Mkuu serikalini ndio nyumba za serikali ziliuzwa kwa bei ya kutupwa, unasemaje kuhusu hili?

Jibu: uuzwaji wa nyumba za serikali, Rais alishauri na Baraza la Mawaziri akakubali. Kuna tume tatu zilifanyia kazi suala hili kwa muda tofauti na zote zilikuja na mapendekezo kuwa nyumba za serikali ni nyingi na serikali inagharamia fedha nyingi kuzikarabati na hivyo tuwauzie watumishi wa Umma.

Tulikuwa na nyumba nyingi mfano Breweries na bandari walikuwa na nyumba zaidi ya elfu moja. Nyumba nyingi zilinunuliwa mpaka na wananchi wa kawaida, Rais alishituka kuona ghorofa zinainuka Oysterbay zilipokuwepo nyumba za serikali.

Rais akasema lazima waraka uandikwe wauziwe wafanyakazi waliokuwa wakiishi humo na hakuna kuuzwa mpaka baada ya miaka 25 kulingana na mkataba wa manunuzi, na serikali ndio ilifanya tathmini na watumishi wa serikali wadogo kabisa wakauziwa.

error: Content is protected !!