December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sumaye, Mwambe hukumu yao Desemba 16

Spread the love

FREDERICK Sumaye na Cecil Mwambe, wanasubiri hukumu yao itayotolewa tarehe 16 Desemba 2019, baada ya kujitosa kugombea nafasi ya uenyekiti-Taifa kupitia Chadema. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Tayari wanachama hao, wameangushwa kwenye uchaguzi wa kanda zao – Sumaye akigombea Kanda ya Pwani na Mwambe Kanda ya Kusini – ambapo sasa, Kamati Kuu ya chama hicho inatarajia kupitisha wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo uenyekiti, makamu mwenyekiti ifikapo tarehe hiyo.

Kwenye nafsi hiyo ya uenyekiti Taifa, Sumaye na Mwambe watavaana na mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe. Mbowe anatetea nafasi hiyo kwa awamu ya nne mfululizo.

Hekaheka na mikakati inaendelea kurindima ndani ya Chadema kuelekea uchaguzi huku ‘kambi’ zikionekana waziwazi.

Taarifa ya kufanyika mchujo huo, imetolewa leo tarehe 3 Desemba 2019 na Tumaini Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema.

“Kamati Kuu ya Chama itaketi tena Desemba 16, 2019, kuteua wagombea wa nafasi za uongozi wa chama ngazi ya taifa,” inaeleza taarifa ya Makene.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi hilo litatanguliwa na uteuzi wa wagombea wa mabaraza ya chama hicho, unaotarajia kufanyika tarehe 7 Desemba mwaka huu.

Wanachama 171 wa Chadema waliochukua, kujaza na kurejesha fomu za kuwania uteuzi wa kugombea nafasi mbalimbali 109  za uongozi wa chama hicho ngazi ya taifa na katika mabaraza, fomu zao zimeshaanza kuchambuliwa.

“Baada ya uchukuaji, ujazaji na urejeshaji wa fomu kukamilika na kuwasilishwa makao makuu ya chama, zoezi la kuzichambua fomu hizo tayari limeanza, vikao vya mchujo na uteuzi vitaanza kwa Sekretarieti ya makao makuu kuketi na kufanya uchambuzi.

Utakaowasilishwa na mapendekezo kwenye kikao cha kamati kuu ya chama, itakayoketi kwa ajili ya kufanya uteuzi wa wagombea wa mabaraza,” inaeleza taarifa ya Makene.

Uchaguzi wa viongozi wakuu wa Chadema unatarajia kufanyika tarehe 18 Desemba 2019.

error: Content is protected !!