October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sumaye ataja sababu zilizomng’oa Chadema

Spread the love

FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza sababu za kurejea CCM leo tarehe 10 Februari 2020, kwamba Chadema walikuwa wamkidharua. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Sumaye aliyepokewa kwenye ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini humo na Dk. Bashiru Ally, katibu mkuu wa chama hicho, amesema, mchango wake ndani ya Chadema umekuwa ukipuuzwa.

Amesema, kwa hadhi aliyokuwa nayo, hakutegemea kama angedharaulika wakati alipokuwa akitoa mchango wake ndani ya chama hicho.

“Huwezi ukawa unatoa mchango tu, kila siku unaonekana wewe labda unashambulia tu, au unafanya nini. Lakini huna sehemu ya kutolea mchango na ukiutoa tu, barabarani kila mtu anakudharau, nikaona mimi si wa hadhi ya kufika kwnye kudharahuliwa.

“Nikasema, mimi nirudi kwenye chama kilichonikuza hadi nikafika pale ambapo leo naweza nikalinga kwamba, nina mchango kwenye taifa hili,” amesema Sumaye.

Amesema, aliamua kuondoka Chadema baada ya kukosa kile alichotarajia kukipata kupitia chama hicho.

“Nimerudi kwa sababu hiyo, matumaini niliyokuwa nimeyategemea kule ya kuweza kuisaidia nchi tu. Mimi shida yangu haikuwa upinzani, ilikuwa nchi tu, mimi ni mzalendo na uzalendo wangu hauwezi kuutilia shaka,” amesema Sumaye.

Sumaye amesema, kwa sasa amerejea CCM kwa ajili ya kukijenga chama hicho pamoja na nchi kwa kushirikiana na wanachama wenzake.

“Nilipoamua kutoka, nilitangaza kwamba sitakuwa kwenye chama chochote kwa sasa. Lakini mimi nilivyosema ni mwanasiasa, ni kazi niliyoifanya maisha yangu yote. Nimekuwa waziri miaka kadhaa lakini nimekuwa kwenye chama na uongozi miaka mingi sana,” ameeleza Sumaye na kuongeza:

“Pia, nitakuwa sitendi haki kama nitajikalia tu mahali, siwezi kutoa ushauri ama mchango wangu katika taifa langu. Nikaona nirudi huko ili kusaidiana na wanachama na wananchi wengine kukijenga chama changu na nchi.”

error: Content is protected !!