July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sumaye amejipa kazi siyo yake

Spread the love

WAZIRI mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amejipa kazi siyo yake. Analenga kupambana na rushwa ndani ya serikali na jamii kwa jumla.

Ni kweli kama anavyosema, Sumaye rushwa ndani ya taifa imeongezeka mara dufu ukilinganisha na utawala wa Mwalimu Julius Nyerere au Benjamin Mkapa.

Shirika la serikali la kupambana na rushwa – TAKUKURU – lililoundwa mahususi kuzuia na kupambana na rushwa nchini, tayari limelemewa na kuna dalili kila dalili limejisalimisha kwa wala rushwa.

Wapo wanaosema, TAKUKURU ni kama imejigeuza taasisi na imejiundia taasisi yake. Yapo madai kuwa taasisi hiyo inajihusisha na vitendo vya rushwa. Hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa moja, lakini hakika rushwa imelishinda shirika hili.

Badala ya kupambana na rushwa, taasisi hii imebaki kulalamika. Hili ni fundisho jingine, kwamba dhambi ikiundiwa taasisi inageuka sehemu ya mfumo wa maisha.

Hata hivyo, kazi hii ambayo Sumaye anataka kuifanya leo, tayari ilimshinda miaka 10 iliyopita – 1995 hadi 2005, wakati akiwa waziri mkuu wa Jamhuri.

Kipindi ambacho Sumaye alikuwa madarakani, ufisadi mkubwa serikalino, ulifanyika wakati utawala wa Benjamin Mkapa na Sumaye ukiwa madarakani.

Kwa mfano, wizi wa fedha za akaunti ya madeni ya nje (EPA), ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ulifanyika wakati Sumaye akiwa waziri mkuu wa Benjamin Mkapa.

Lakini mlipuko wa taarifa za ufisadi ziliibuka baada ya yeye na Mkapa kung’atuka. Kwa mtindo huo, kashfa ya ufisadi kama ile ya kampuni ya kitapeli ya kufua umeme wa dharula ya Richmond Development Company (RDC), ilipoibuka na kufahamika.

Mkataba huu ulilalamikiwa na baadaye kuthibitishwa kuwa utoaji zabuni kwa kampuni hiyo ulikuwa umegubikwa na upendeleo na hivyo kukiuka taratibu.

Mchakato wa zabuni ulihusisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye, baada ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge, alilazimika kujiuzulu.

Mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, walijuzulu pia kutokana na kashfa hiyohiyo.

Aidha, mikataba ya kuchimba madini pamoja, ukiwamo unyonyaji katika mkataba wa kuzalisha umeme wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya, yote ilifanyika wakati wa Sumaye akiwa waziri mkuu.

Unaweza kujiuliza kwa nini basi Sumaye hakuupigia kelele ufisadi wa aina hiyo wakati huo?

Mkataba mkataba kati ya serikali na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ulifungwa wakati wa utawala wa rais Ali Hassani. Mkataba huo wa miaka 20, kuanzia 1995 ulipashwa kufikia tamati mwaka 2015 kwa IPTL kukabidhi mitambo hiyo kuwa ya umma.

Lakini katika mazingira ya kutatanisha, mwaka huu, yaani mwaka mmoja kabla ya Serikali kukabidhiwa, mitambo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan-African Power Ltd, ambayo sasa imo mbioni kuingia Mkataba na TANESCO wa kuuziana umeme chini ya masharti kama yale ya IPTL.

TANESCO iligundua mapema ulaghai wa IPTL kwenye mkataba na kufungua kesi mwaka 2001, lakini ikashindwa baada ya kubainika kuwa vigogo wa chama tawala na serikali walijua mapema na kuridhia mkataba huu kuendelea chini ya ulaghai huo.

Utawala wa Mkapa na sasa huu wa Kikwete, hauwezi kukwepa lawama za kushiriki kuangamiza taifa katika suala hili.

Kashfa ya IPTL, ambayo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), liliita “mzigo usiobebeka kwa uchumi wa Tanzania,, iliashiria unyonyaji usiovumilika unaofanywa na kikundi kidogo cha watawala. Serikali ya Rais alinywea. Sumaye alinyamaza. Aliufyata.

Katika muktadha huo, Sumaye hana mamlaka ya kuzungumzia tatizo la rushwa nchini. Hana. Ni kwa sababu, mfumo wa rushwa umeasisiwa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Umekumbatiwa na viongozi wakuu wa serikali wa sasa na wa wakati huo.

error: Content is protected !!