October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sumaye ajitosa kumkabili Mbowe

Spread the love

LICHA ya “vitimbi” vya wafuasi wa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye, bado ameendelea kujitosa katika kinyang’anyiro cha uenyekiti huo. Anaripoti Bupe Mwakiteleko … (endelea).

Sumaye ambaye amepata kuwa waziri mkuu wa Jamhuri kwa miaka 10 mfululizo – 1995 hadi 2005 – alirejesha fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema, leo tarehe 30 Novemba 2019, makao makuu ya Chadema, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Fomu ya Sumaye ilirejeshwa na Mustafa Muro, diwani wa Kata ya Kinondoni; siku mbili baada ya kuangushwa katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Kanda ya Pwani.

Huku kukiwa na madai ya kushindwa katika uchaguzi huo ambako alikuwa mgombea pekee, Muro alisema, “…mheshimiwa Sumaye amejipanga kukabiliana na hujuma kutoka kwa makundi yasiyomuunga mkono.”

Alisema, “Leo hii nimerudisha fomu yake ya uenyekiti ngazi ya taifa. Tunagonjea hatua ya kuteuliwa ili tuanze na kampeni.”

Aliongeza: “Lakini kisisasa tunaamini hiki ni chama cha demokrasia na maendeleo, tunaaamini kwenye demokrasia. Tunajua kuna watu wanafanya siasa za makundi, lakini safari hii tutapambana, na tutashinda sababu ukiona mtu anafanya figisu ana mashaka na hivyo anakuogopa.”

Akizungumza na MwanaHALISI, kwa njia ya simu mara baada ya kurejesha fomu hadi kuwania nafasi hiyo, Sumaye alisema, “pamoja na kwamba niliadhibiwa kwa sababu ya kutaka kugombea nafasi hii, lakini bado ninaendelea kugombea.”

Sumaye alisema, “ninakwenda kugombea kwa kuwa ni haki yangu ya kikatiba.” Akijibu swali la kwamba haoni kuwa na huko ataadhibiwa kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa Kanda ya Pwani, Sumaye alisema, “nimejiandaa kwa hilo.”

Sumaye aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu wa Kanda ya Pwani, Alhamisi iliyopita, tarehe 28 Novemba, kwamba ni kweli aliamua kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, lakini hajaijaza na hivyo anaweza kuirejesha au kuichana.

Sumaye alishindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Pwani, baada ya kupigiwa kura nyingi za  hapana.  

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kibaha zinasema, kushindwa kwa Sumaye, kumesukumwa na uamuzi wake wa kugombea uenyekiti wa Mbowe. 

Taarifa zinasema, wapambe wa Mbowe, wakiongozwa na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob Mwangombola, walifika Kibaha na kuwaficha wajumbe hotelini na kuwashawishi wampigie kura za hapana mwanasiasa huyo.

Wakati Sumaye akirudisha fomu yake leo, mshindani wake wa Mbowe amerudisha fomu ya kutetea nafasi hiyo kupitia kwa Amani Golugwa, katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini.

error: Content is protected !!