Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa SumaJKT yaokoa mamilioni ya Serikali
Habari za SiasaTangulizi

SumaJKT yaokoa mamilioni ya Serikali

Spread the love

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa vituo saba vya umahiri na jengo la mafunzo kwa wachimbaji wadogo katika Chuo cha Madini Dodoma ambapo miradi hiyo itagharimu Sh. 11.9 bilioni hadi kukamilika kwake. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Usainishaji mikataba hiyo ulifanywa kati ya Wizara ya Madini na Kampuni ya SUMAJKT ambao ndiyo itakayojenga vituo hivyo kuanzia Julai na kukamilisha Desemba mwaka huu huku sh. 249.3 milioni zikiokolewa kwa kutumia kampuni hiyo ya jeshi.

Akizungumza mara baada ya kutiliana saini mikataba hiyo, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema wameamua kutumia kampuni ya SUMAJKT kutokana na kujiimarisha kwao na kupatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kwa kiasi kikubwa uwezo wao kiufundi katika kutekeleza miradi mikubwa kwa wakati, ubora wa kazi zao na gharama nafuu ndicho kimewezesha Serikali kuwapatia kazi hiyo.

Alibainisha kuwa kampuni hiyo iliwahi kupewa kazi ya ujenzi wa ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5 kuzunguka mgodi wa Tanzanite, Mererani na kukamilisha kwa wakati.

“Kama mtakavyoshuhudia leo mikataba ikisainiwa wizara imeajiri kampuni ya ujenzi ya SUMAJKT kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo ambayo inajihusisha na kazi mbalimbali ikiwemo kazi za ujenzi.

Serikali imewamini na inawaamini kuwa kazi hii mtaifanya kwa ubora unaostahili na kukamilika kwa wakati kwa kuzingatia mikataba itakayosainiwa leo, kazi hii itasimamiwa na washauri elekezi ambao ni kampuni ya Y&P Architects ambayo imesanifu majengo ya Songea, Mpanda na Chunya.”

Amesema kampuni ya Interconsult LTD ambayo imesanifu majengo ya MRI na Handeni na Kampuni ya SKY Architects ambayo imesanifu majengo ya Musoma, Bukoba na Bariadi.

Aliongeza kuwa ni imani yao kuwa ifikapo Desemba 2018, mtatukabidhi majengo yaliyokamilika kwa ajili ua matumizi

Awali Waziri Kairuki alifafanua kuwa ujenzi huo wa majengo ya ofisi saba za madini ili kutumika kama vituo vya umahiri vya masuala ya madini.

“Mtakumbuka wakati nawasilisha bungeni mpango wa fedha wa mwaka 2018/19 nililieleza bunge na wananchi kuwa katika mwaka huu, Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya ofisi saba za madini ili zitumike kama vituo vya umahiri vya masuala ya madini,”alisema.

Waziri huyo alizitaja ofisi hizo kuwa ni pamoja na Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, Bariadi, Bukoba na Musoma.

“Serikali itafanya upanuzi wa miundombinu ya Chuo cha Madini Dodoma kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa na chama cha wachimbaji madini wanawake.

“Hivyo ninayo furaha kuwataarifu kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo umeanza rasmi na leo tumesaini mikataba kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo hayo,” amesema.

Waziri Kairuki amesema ujenzi wa vituo hivyo unatekeleza kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali madini.

Amesema  moja ya malengo mahsusi ya mradi huo ni kuboresha manufaa ya sekta ya madini nchini hususani kusaidia wachimbaji wadogo ili kuwaongezea ujuzi katika eneo la uchimbaji madini na kukuza uchumi wao.

Amesema katika vituo hivyo kutakuwa na vyumba vya madarasa, ,mikutano, maktaba kwa ajili ya taarifa mbalimbali pamoja na maabara zitakazotumika katika utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo.

“Mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali madini umetekelezwa kwa awamu mbili wa mkopo kutoka benki ya dunia,” amesema Waziri Kairuki.

Amesema awamu ya kwanza ya mradi ilitekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Septemba 2009 hadi Juni 2015 na kwamba ya pili imeanza kutekelezwa kuanzia Septemba 2015 na utakamilika Desemba mwaka huu.

Alitaja mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa mradi katika awamu ya kwanza ambayo ni uwezeshaji wa Serikali kupata nyongeza ya mkopo kutoka benki ya dunia ili kutekeleza kazi nyingine muhimu katika sekta ya madini zikiwemo ujenzi wa vituo vya umahiri na mfano.

Alisema vituo hivyo vitatoa mafunzo ya jiolojia hususani katika utafiti wa madini. Mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususani zisizotumia kemikali ya Zebaki.

Vilevile, vituo hivyo vitatoa mafunzo ya biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora ya utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Mhandisi Morgan Nyonyi alisema kuwa tukio hilo linapiga hatua kwenye utekelezaji wa mradi huo na kwamba wao kama wakandarasi wa mradi huo wamejipanga kuhakikisha unatekelezwa kwa muda uliopangwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!