May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sukari imetusahaulisha Lugumi?

Spread the love

SAKATA la kukosekana sukari limeshika kasi nchini.Tatizo la kukosekana sukari lilianza baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ya nchi kwa kile alichosema ni kulinda viwanda vya ndani. Je suala hili la Sukari limetusahaulisha sakata la Lugumi? Anaandika Josephat Isango.

Yawezekana nia ya Magufuli ilikuwa nzuri kwa kuitamka lakini tayari wasomi wamemkosoa. Uamuzi wa Magufuli wa kuzuia sukari kutoka nje ya nchi sasa unaonekana ulikuwa wa kukurupuka.

Tayari msomi na mataalamu wa masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Semboja Haji amesema msimamo huo wa Magufuli ni kinyume na makubaliano ya mkataba wa kimataifa juu ya bidhaa hiyo.

Magufuli ameshawatangazia watanzania kuwa watu wanaotuhumiwa kwa makosa hayo wafikishwe mahakamani, kumbe sheria inasema wakipatikana na tuhuma hizo hupelekwa kwenye bodi ambayo ndio inatambulika.

Kimsingi, serikali ya Chama cha Mapinduzi, kinara wake Magufuli wamesababisha tatizo la sukari nchini, sasa wanavamia maghala ya wafanyabiashara binafsi na kuwalazimisha kuuza au tunaarifiwa inagawiwa bure. Bila shaka hiyo itakuwa sukari ya watu walioingiza kimagendo au kwa mianya mibovu ndo wanaweza kukumbwa na hatia hizo.

Katika ulimwengu huu wa soko huria, mfanyabiashara aliyeagiza sukari kihalali, akalipia kodi anauza kwa wateja wake, sijui kama Magufuli anaweza kuingilia vile. Ni biashara ya kawaida hata ukienda mikoani sasa wakati wa mavuno watu wananunua mazao wanaweka na ikifika wakati fulani wanauza. Kila mfanyabiashara anahitaji faida na wapo wanafanya vile kwa mitaji ya kukopa.

Kwa hiyo wanakopa wanaleta sukari lakini serikali inagawa bure sababu ya kuadimika sukari nchini kulikosababishwa na amri ya Rais ya kuzuia kuingiza sukari nchini.

Serikali inapaswa kuwa na uwezo wa kuagiza sukari katika ulimwengu wa biashara huria ili kutojiingiza katika mgogoro na wafanyabiashara kusulubu wananchi, kwa sababu tatizo ambalo kwa upande mwingine inaonekana serikali imechangia.

Bajeti za wizara mbalimbali mjini Dodoma zinaendelea kusoma, na wiki iliyopita tumesomewa bajeti ya Wizara ya viwanda Biashara na Uwekezaji.

Makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa 2016/17 kati ya fedha hizo, Sh 53.5 bilioni (sawa na asilimia 56), zimetengwa kwa matumizi ya kawaida wakati Sh42.1 bilioni (asilimia 44) ni kwa ajili ya maendeleo.

Nimechukua mfano wa Wizara hiyo kukumbushia kiwango cha pesa zilizokwapuliwa na vigogo kadhaa katika sakata la mkataba wa Lugumi na jeshi la polisi.

Kiwango cha pesa zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ya bajeti ya Viwanda, Biashara na uwekezaji zinazidi kwa bilioni 7 tu za pesa za Lugumi. Naamanisha Lugumi tunaambiwa pamoja na wenzake walikwapua bilioni 35 katika mkataba wenye utata, lakini Wizara imetengewa pesa za maendeleo bilioni 42.

Kwa maana hiyo bajeti ya maendeleo ya Wizara hiyo inakaribiaana sana na pesa zilizochukuliwa na watu wachache. Magufuli amekasirishwa na mambo mengine ila hili analikwepa. Je Magufuli anatambua kuwa sakata la Lugumi ni jipu? Anaogopa kuligusa? Kwanini.

Takribani mwezi na nusu sasa kuna kitu kinaitwa Lugumi. Askari Polisi wengi wanafahamu jina la Lugumi sababu limehusishwa na Said Mwema Mkuu wa Jeshi hilo aliyestaafu muda si mrefu, Waandishi wengi wameliandika jina la Lugumi au kulitaja au kulisoma kwenye taarifa mbalimbali.

Wananchi mtaani wamesikia katika redio au televisheni linavyojadiliwa, bunge na serikali zimetupiana mizigo kana kwamba hili jina la Lugumi, haligusiki, likitajwa kwenye ofisi za polisi na serikali ya CCM masikio yanawasha, wote wameliogopa.

Hata matapeli mtaani wameshalisikia jina la Lugumi, na kushangaa uwezo wa jeshi la polisi katika fikra hadi wakaingizwa kwenye mkataba ambao sasa wanaogopa kuutoa. Kama Polisi wanakuwa na mikataba tata wanapata wapi uhalali wa kukamata, kuchunguza na kuwasweka rumande wengine wenye mikataba tata?

Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na Bunge wameshindwa kuwajibika kwa wananchi kuhusu suala la Lugumi, wamebaki kutisha waandishi wa habari, wamebaki kutengeneza danadana, majibu tofauti kila siku. Leo husema hiki kesho kile.

Bunge la Jamhuri ya Muungano sasa linatuhumiwa kuwa kizingiti kikubwa kukwamisha suala la Lugumi lisijadiliwe, na hadi sasa kamati iliyoundwa imeshindwa kufanya kazi yake kuweka wazi ubadhirifu huo wa pesa za wananchi kupitia mkataba wenye utata.

Tumekuwa mabingwa wa kusahau masuala muhimu katika nchi sababu tunaenda kimatukio matukio, suala la Dowans ilipwe au isilipwe, ni ya nani? Ya mtanzania au si ya mtanzania liliuawa na kuibuka kwa babu wa Loliondo, sasa hivi ukiuliza Dowans ililipwa au haikulipwa hata baadhi ya waandishi hawajui. Ilikuwa ya nani imebaki hadithi tu.

Suala la Wizi wa EPA kwa sasa limeshasahaulika, wezi wamesahaulika, waliokwapua katika tuhuma kama meremeta, Mwananchi, na mingine sasa imebaki historia nchini kwetu.

Sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa vibaya Dk Ulimboka Stephen, hata suala la Joshua Mulundi sasa hayakumbukwi tena.

Kumetokea vituko vingi sana, mara homa ya dengue na tukaambiwa watu kadhaa wamefariki, mabasi yakapulizwa dawa na ugonjwa ukaonekana ni hatari ili kuzuia maandamano ya Chadema, na chuki za wananchi dhidi ya sakata la ukwapuaji wa pesa za escrow, yamepita yamebaki historia.

Kwa sasa tuhuma kedekede za Lugumi, ambazo kunaonekana kuwa pesa zilipigwa na wajanja, limeacha kuzungumza, hata Magufuli hakulizungumzia hata tone, licha ya kukemea uhalifu na kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu amenyamazia hela hizo zinazokaribia na bajeti ya Wizara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ila akaona nafuu achukue hatua kwa Wilson Kabwe, Mkurugenzi wa Jiji kwa upotevu wa bilioni 3.

Magufuli hajataka hata kukumbuka kuwa Paul Makonda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anafanya kazi kisiasa, kuhadaa watu. Magufuli alipaswa ajiulize sakata la Waalimu kusafiri Dar limefia wapi kabla hajamwamini Makonda.

Kuishi kwa matukio hivi kutasababisha tusahau sakata la Lugumi, limekuwa na vituko tangu lilipoanza kutajwa, jinsi Ernest Mangu Mkuu wa jeshi la polisi na Projestus Rwegasira Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani walivyotupiana mpira wasipeleke mkataba kwenye kamati ya Bunge, jinsi danadana ilivyotokea kati ya Wizara na Bunge, jinsi sarakasi zilivyotokea hadi ikaundwa kamati ya wabunge tisa ambao hadi sasa hawasikiki. Sasa sakata la sukari limesababisha Lugumi sio habari tena hata kwenye vyombo vya habari, serikalini na bungeni. Taifa la ovyo!

error: Content is protected !!