May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sugu ampa ujumbe Kikwete

Spread the love

 

ALIYEKUWA Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’, amemuomba Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, kutumia busara zake kuliunganisha Taifa, kama alivyofanya nchini Zambia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Sugu ametoa ombi hilo jana Jumatatu tarehe 16 Agosti 2021, kupitia ukurasa wake wa twitter, baada ya Kikwete kuwapatamisha waliokuwa wagombea wa urais wa Zambia, katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, uliofanyika tarehe 12 Agosti 2021.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Sugu amemuomba Kikwete atumie busara zake kuliunganisha Taifa, akidai hali si shwari, kuanzia kwenye Chama chake Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, Sugu hakutaja masuala yaliyosababisha nchi kutokuwa shwari. Ingawa kwa sasa Chadema ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, kinapitia katika misukosuko baada ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kuwa rumande katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, kwa zaidi ya wiki tatu.

Anakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini humo.

“Hongera sana mzee Kikwete, kwa upatanishi huko Zambia. Ukirudi na nyumbani tunakuomba utumie busara hizo hizo na ufanye jambo, maana hali si shwari kuanzia ndani ya chama chako mpaka kwetu sisi. Nchi inazidi kuwa na tete, tukumbuke hakunaga mshindi kwenye ugomvi wa familia,” ameandika Sugu.

Katika uchaguzi huo nchini Zambia, aliyekuwa Mgombea Urais wa upinzani kupitia Chama cha United Party for National Development (UNDP), Hakainde Hichilema, alitangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi Zambia (ECZ), baada ya kupata kura 2,810,777.

Hichilema alimbwaga Rais aliyemaliza muda wake kupitia chama cha Patriotic Front (PF), Edgar Lungu, ambaye amepata kura 1,814,201.

Kufuatia matokeo hayo, Lungu alikubali kushindwa na kutangaza kuwa yupo tayari kumkabidhi ofisi Hichilema.

Kikwete alikuwa ni mmoja wa waangalizi wa uchaguzi huo, kupitia Jumuiya ya Madola. Siku moja baada ya kutangazwa mshindi, jana tarehe 16 Agosti 2021, Rais Mteule wa Zambia, Hichilema aliwashukuru waangalizi wa uchaguzi, akiwemo Kikwete.

error: Content is protected !!