October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sudani kwalipuka tena

Spread the love

MAELFU ya raia wa Sudani, wamerudi mtaani kufanya maandamano upya wakisema, walichokitaka kwenye maandamano ya awali, hakijafanikiwa. Inaripoti mitandao ya kimataifa … (endelea).

Licha ya kuwepo kwa tishio la virusi vya corona, wananchi hao wameanza maandamano jana tarehe 30 Juni 2020, wakidai mabadiliko zaidi yanayoendana na matakwa yao ya awali.

Maandamano yalilipuka mwaka jana na hatimaye Omar al-Bashir, aliyekuwa rais wa taifa hilo takribani kwa takriban miaka 30, aling’olewa na kutiwa mbaroni.

Waandamanaji wameingia mitaani wakidai matarajio yao ya haki, usawa na maisha bora bado hayajafikiwa licha ya kufanya mapinduzi na kuong’oa utawala wa al Bashiri.

Na kwamba, haki ya waandamanaji waliopoteza maisha yao kwenye maandamano tangu Desemba 2018 yalipoanza, bado haijaonekana.

Wanadai, serikali ya mpito ilichofanya ni kupokea nyaraka tu na kukabidhi jeshi, jambo ambalo kwenye utawala wa maridhiano halina maana kwa mazingatio ya madai yao ya maisha bora ambayo hayajashuhudiwa.

Wakipeperusha bendera ya taifa hilo, waandamanaji walikusanyika mjini Khartoum, Khartoum ya Kaskazini na Omdurman baada ya serikali kufunga barabara na madaraja ili kuzuia maandamano kuendelea kusambaa.

Polisi wanaripotiwa kutumia maji ya kuwasha ili kutawanya waandamanaji waliokuwa wamejaa kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa Khartoum.

Maandamano hayo pia yamefanyika katika Mji wa Kassala uliopo Mashariki mwa Sudan na Darfur. Waandamanaji wamekuwa wakitumia maneno haya “Uhuru, Amani na Haki”, kulazimisha serikali ya mpito kutekeleza kiini cha maandamano yao ya awali.

Baadhi ya waandamanaji wamekuwa wakichoma moto matairi ikiwa ni sehemu ya kuonesha hasira zao kwa serikali ya mpito.

error: Content is protected !!