January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Subira yachosha Z’bar

Spread the love

MWENENDO wa mambo kuhusu mgogoro wa uchaguzi ulioibuka Zanzibar unazidi kukatisha tamaa wananchi hasa kwa kuhofia ukimya kutawala badala ya hatua za wazi za utatuzi. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Tangazo la Serikali linalolenga kuhalalisha uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, wa kufuta uchaguzi nalo limeongeza utata na kuzusha hisia kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepindua maamuzi ya wananchi.

Wazanzibari walipiga kura Oktoba 25 kuchagua Rais, Wawakilishi na Madiwani, pamoja na rais wa Jamhuri na wabunge, lakini wakati matokeo ya jamhuri yametambuliwa, yale ya viongozi wa Zanzibar yamefutwa.

Hoja ya kufutwa imepingwa na washiriki wengi na kulalamikiwa na nchi wafadhili waliotuma wawakilishi wao katika uangalizi wa uchaguzi huo.

Asasi za waangalizi wa ndani na kimataifa zimesema uamuzi wa kufuta uchaguzi ni kosa kubwa lisilotarajiwa kwa kuwa uchaguzi ulisimamiwa vizuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2010.

Jecha aliufuta uchaguzi wakati tayari Maalim Seif Shariff Hamad, aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), alishatangazia ulimwengu siku mbili kabla, mwelekeo wa kupata ushindi wa asilimia 52.87 ya kura dhidi ya 47.13 za Dk. Ali Mohamed Shein.

Uamuzi wa Jecha umechapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Novemba 6, mwaka huu, ambalo hata hivyo, ni jana tu ndio lilienezwa kwa “nguvu kubwa” juzi na kupigiwa chapuo na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, umefutwa kwa sababu ya matatizo mbalimbali yaliyotokea.

Kwa mara nyingine, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimesema tangazo hilo linaongeza ugumu wa utatuzi wa mgogoro kwa kuwa linaendeleza uharamu wa uamuzi wa Jecha uliotolewa pasina nguvu yoyote ya kisheria.

Katibu wa ZLS, Omar Said Shaaban amesema tangazo hilo ni mbinu tu za CCM kulazimisha hoja zake ambazo zimeshindwa mbele ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Na. 11 ya 1984 na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

“Hapa ingefaa kutokea mwananchi akachukua hatua ya kupinga masuala haya kwa kufungua shauri kwenye mahakama. Utata utaondoka,” alisema katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) jana mchana.

Hoja hiyo inazidi kuthibitisha uharamu wa hatua ya Jecha, ambaye Oktoba 28, huku akiwa ameshatangaza matokeo ya urais ya majimbo 31, alitangaza kufuta uchaguzi mzima.

Anatajwa kuwa alifanya hivyo kwa uamuzi wa peke yake, kwa kuwa baadhi ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi, walijitokeza na kupinga hatua yake.

Akizungumzia tangazo la serikali la Novemba 6, rais wa ZLS, Awadh Ali Said amesema kuwa halihalalishi kilichoharamika mapema kwa kuwa msingi wake ni kutokuwepo mamlaka ya kisheria ya kufutwa uchaguzi na mwenyekiti Jecha wala Tume yenyewe.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika wasaidizi wa Dk. Shein, ndiye anayechochea hatua zinazoongeza utata wa mgogoro uliopo akishirikiana na baadhi ya wahariri katika Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Tangazo hilo linaloelekeza kuwa kutakuwa na uchaguzi mwingine hapo baadaye, limetengenezewa kipindi maalum kupitia ZBC ambacho wengi wanakiona kama kinacholenga “kuongeza kuliko kupunguza mkanganyiko katika mgogoro.”

Vyombo vya habari vya SMZ ambacyo vilikuwa kimya kuhusu kinachoendelea tangu kufutwa kwa uchaguzi, vimeibuka na kulidaka tangazo hilo hata kulitolea tahariri.

Wahariri wake wamechukua msimamo wa kunyamazia taarifa za kuwepo vikao vya viongozi wakubwa wa Zanzibar vinavyofanyika Ikulu vikimshirikisha Rais Dk. Shein.

Maofisa wa Ikulu nao wamegoma kuzungumzia hata kwamba kunafanyika vikao hivyo – kimoja kikianza Jumatatu na kuendelea juzi Jumatano.

Marais wastaafu walioshiriki vikao hivyo ni Ali Hassan Mwinyi aliyetoka 1985 na Amani Abeid Karume aliyetoka 2005 baada ya kuongoza kwa miaka kumi. Naye Dk. Salmin Amour Juma, aliyeongoza kwa miaka kumi kufikia 2000, alihudhuria kikao cha Jumatano. Katika hatua nyingine, wakati tangazo hilo linapingwa na wanasheria, huku likishikiliwa bango na serikali iliyo katika udhibiti mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali haijaeleza lolote kuhusiana na vikao hivyo vya faragha.

Rais Dk. Shein ameshiriki vikao hivyo pamoja na makamu wake wawili, Balozi Seif Ali Iddi wa CCM, na Maalim Seif anayepigania haki ya kuongoza Zanzibar kwa kuamini kuwa amepewa ridhaa na wananchi kwa njia ya kura.

error: Content is protected !!