August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

SUA yasonga mbele utafiti wa kilimo

Spread the love

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia shule yake ya Uchumi Kilimo na Stadi za Biashara kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ergaton cha Kenya, wamezindua mradi wa utafiti kuhusu tija ya uzalishaji, ubora wa mbegu kijenetiki na lishe ya mama na motto, anaandika Christina Raphael.

Utafiti huo unalenga kusaidia takwimu sahihi za matumizi ya mbegu bora na kuondoa udumavu kwa kuhakikisha lishe bora na afya bora kwa wananchi vinakuwepo.

Mradi huo utatekelezwa kwa ufadhili wa wa taasisi ya Bill na Melinda Gates, katika wilaya 23 zilizoko kwenye mikoa 11 ya kanda tatu za Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kusini,

Prof. Damian Gabagambi, Mkuu wa shule ya Uchumi Kilimo na Stadi za biashara ya SUA amesema, ingawa takwimu za matumizi ya mbegu bora zimekuwepo, bado hazina uhakika wa kutosha kutokana na kuzipata takwimu hizo kwa kuwahoji wakulima.

Amesema, nchi nyingi duniani zilibaini kuwa ni asilimia 20 tu huwa takwimu za kweli zinazohusisha wakulima katika kufahamu iwapo kweli wanatumia mbegu bora za kilimo.

Hivyo, shule hiyo kwa kushirikiana na Ergaton wameamua kufanya utafiti utakaohusisha kupata vinasaba vya mbegu zinazotumiwa na wakulima.

Amesema, lengo ni kubaini mbegu wanazotumia kama kweli ni za kisasa au za kienyeji kama wanavyokuwa wamejieleza katika mahojiani.

“Tunakwenda kuwauliza wakulima maswali kama walivyozoea, lakini tutakwenda kuchukua sampuli za mbegu wakati wa uvunaji na kutenganisha vinasaba ili kujua kama kweli mbegu hizo ni za kienyeji au kisasa kama walivyojieleza,” amesema na kuongeza;

“Lengo ni kupata takwimu sahihi, hata mbolea ikipelekwa iendane na mbegu bora, maana mbolea haikubali kwa mbegu za kienyeji, inaendana na mbegu bora za kisasa, na matokeo haya tunaamini yatasaidia Serikali katika kutunga sera zake za kilimo.”

Akizindua rasmi mradi huo kwa niaba ya serikali, Dk Florence Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema, mbegu ni muhimu katika shughuli zote za kilimo.

Amesema, zimekuwa zikionesha mwelekeo na hali ya mavuno, lishe, namna ya kuongeza thamani, uhimili wa magonjwa na ukame na kwamba, bila mbegu hakuna lolote linaloweza kufanyika kwenye kilimo.

Amesema, kutokana na uhumimu huo, serikali imeendelea kufanya juhudi kuhakikisha inaongeza tija ya uzalishaji wa mazao kwa kuanzia na mbegu bora, kwa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora sambamba na mahitaji mengine kwenye kilimo ikiwemo mbolea na viuatilifu.

Dk Tutuka amesema, kupitia utafiti huo, serikali na wadau wengine wataweza kupata taarifa sahihi za matumizi ya mbegu bora katika kilimo.

error: Content is protected !!