CHUO kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani hapa kinajipanga kuboresha mbinu za ufundishaji kwa vitendo ili kuwafanya wahitimu kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kutembea mitaani kutafuta ajira. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala SUA, Prof. Amandus Muhairwa alisema hayo jana tarehe 1 Mei 2023 wakati wa uzinduzi wa kamati ya Ushauri wa viwanda na kuzungumza na watekelezaji wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano SUA mkoani hapa.
Prof. Muhairwa ambaye pia ndiye mratibu wa mradi wa HEET alisema SUA imepokea kiasi cha Dola za kimarekani 32 bilioni ambazo ni sawa na Sh. 73.6 bilioni na kati ya fedha hizo Sh. 55.2 bilioni zitatumia katika Chuo cha SUA -Morogoro na Sh. 18.4 bilioni zitatumika katika kampasi SUA – Katavi.
Prof. Muhurwa alisema pia kutakuwa na vifaa na mitambo ya kilimo, ujenzi, vifaa vya uzalishaji vya kumfanya wanafunzi kujifunza zaidi, mtambo wa kutafiti na kutunza maji kwa watu wa digrii mbalimbali ikiwemo uhandisi kilimo, kuimarisha karakana na sehemu za kujifunzia, tingatinga litakalotumika katika kusafisha mashamba sambamba na kuanzisha mitaala mipya na kuhuisha mitaala 108 iliyopo ili kuwezesha wahitimu kujiajiri na kuajiri, kuongeza mbinu bunifu za ufundishaji sambamba na kujenga uwezo wa watumishi kielimu.
Alisema mpaka sasa wanataaluma 41 wa shahada za umahiri na uzamivu wanaendelea na masomo katika vyuo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe alisema mradi huo umepata mkopo nafuu wa fedha kiasi cha dola za kimarekani 425 milioni ambazo ni sawa na zaidi ya Sh. 972 bilioni kutoka benki ya dunia ambao unatekelezwa kwa miaka 5 kuanzia 2021/26 ukihusisha vyuo vikuu 14 vya umma, taasisi zilizopo chini ya elimu zinazoshughulika na elimu ya juu ikiwemo CPU na COSTECH na Taasisi tano kutoka Wizara ya fedha.
Naye Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Kaboko Mkalinga aliwataka waajiri kujitoa vema katika utekelezaji wa mradi huo kutokana na uzoefu walionao na kuhakikisha wanatoa mchango wao kwa wananchi ili mradi huo ufanikiwe kwa kutengeneza uzalishaji wa ajira nchini.
Leave a comment