July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Stika mpya kuhusu albino yaja

Viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS) walipozungumza na Rais Jakaya Kikwete

Spread the love

TAASISI ya Albino Enterprises of Dar es Salaam inatarajiwa kuzindua stika maalum yenye ujumbe wa kuhamasisha umma kukomesha mauaji ya watu wenye albinism nchini. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Stika hiyo pia itahusu kampeni ya kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya ngozi inayowakabili watu wenye albinism kwa sababu ya ngozi yao kuathiriwa na mionzi ya jua.

Uzinduzi wa stika hiyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Michael Lugendo, umepangwa kufanyika 26 Januari mwaka huu Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police Station), jijini Dar es Salaam.

Lengo la kutoa stika hiyo ni kuhamasisha Watanzania kuungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli na Jeshi la Polisi katika kuchukua hatua za kupambana na hatimaye kutokomeza mauaji hayo.

Lugendo amesema taasisi yao mbali na kuhamasisha ukomeshwaji wa vifo vya maalbino vinavyotokana na kukatwa viungo, bali pia vifo vinavyosababishwa na saratani ya ngozi inayotokana na maalbino kukosa mafuta ya kuzuia athari za mionzi ya jua.

“Kulingana na kasi ya mabadiliko ya tabia ya nchi, sisi albino ni wahanga wakubwa na jamii isipochukua hatua za makusudi upo uwezekano wa watu wenye albinism kuangamizwa na saratani ya ngozi kwa kuwa wengi wao ni masikini wasiomudu kupata mafuta ya kujisaidia kujikinga na athari za mionzi ya jua,” amesema.

Amesema katika ulingana na changamoto hii hatari wanayokutana nayo ya kuathirika na mionzi ya jua hadi kupelekea saratani ya ngozi wameamua kuchukua hatua mapema,pia taasisi imemteua mchezaji wa kimataifa Mbwana Ally Samata kuwa balozi wa kudumu wa kusemea watu wenye albinism na majukumu yake kiujumla ni kuhamasisha dunia kwa njia ya soka kuhakikisha kwamba hakuna mlemavu wa ngozi anayefariki tena kwa kifo cha saratani ya ngozi na mauaji ya kukatwa viungo yanayotokana na imani za kishirikina.

Stika itakayozinduliwa itasambaza nchi nzima ambako itabandikwa kwenye magari, bajaji, pikipiki, maofisini, majumbani, madukani na masokoni, kumbi za starehe na vituo vya usafiri wa umma.

Amesema taasisi hiyo itatoa elimu mikoa ya maeneo ya Kanda ya Ziwa ambako tatizo la mauaji ya maalbino limekuwa kubwa. Mikoa hiyo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora na Mara.

Lugendo ameomba wakurugenzi wa kampuni na asasi mbalimbali kujitokeza kuunga mkono uzinduzi wa stika hiyo ikiwemo kudhamini kwa kusaidia kufanikisha uzinduzi.

Amesema upo umuhimu wa kila mwananchi kushiriki kusaidia kampeni ya kutokomeza mauaji ya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa kujitolea taarifa zitakazowezesha kufichua mipango ya wanaoshiriki mauaji hayo.

error: Content is protected !!