January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Stars kuwavaa Algeria Novemba 14, Ligi Kuu kesho

Spread the love

MECHI ya hatua ya pili kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi kati ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Algeria ‘The Fox Desert’ utafanyika Novemba 14, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager itacheza mchezo huo dhidi ya Mbweha wa Jangwani siku ya Jumamosi Novemba 14, na mchezo wa marudiano kuchezwa siku tatu baadae Algeria 17 Novemba, 2015.

Kikosi cha Stars chini ya Kocha Mkuu Charles Mkwasa kimefanikiwa kusonga hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Malawi (The Flames) kwa jumla ya mabao 2-1, nyumbani ikishinda 2-0, na kufungwa 1 – 0 jijini Blantyre.

Wakati huohuo, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, ikiwa katika mzunguko wa saba timu 14 zitapambana kusaka pointi 3 muhimu.

Young Africans watawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi, huku timu zote zikiwa na pointi 15 kileleni zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa.

Kabla ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam, kutakua na mchezo wa utangulizi wa kuombea amani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, 2015.

Mchezo huo utawakutanisha viongozi wa dini watakocheza dhidi ya mabalozi wanaofanya kazi nchini, mechi hiyo itaanza saa 8:25 mchana na kumalizika saa 9:15 alasiri.

Majimaji FC ya mkoani Ruvuma watakua wenyeji wa African Sports kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea, huku Ndanda FC wakiwakaribisha Toto African kutoka jijini Mwanza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Jijini Mbeya, watoza ushuru wa jijini hilo Mbeya City FC watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine, Chama la wana Stand United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Coastal Union wagosi wa kaya wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa michezo miwili kuchezwa, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakwani, huku Mwadui FC wakicheza na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Mwadui Complex.

error: Content is protected !!