August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

SSRA yasisitiza miongozo yake kufuatwa

Irene Isaka, Mkurugenzi SSRA

Spread the love

MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imewataka watendaji wa mifuko hiyo kufuata kanuni na taratibu za uandikishaji kwa mujibu wa mwongozo wa mamlaka hiyo, anaandika Christina Haule.

Wito huo umetolewa leo mkoani Morogoro na Sarah Msika, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano SSRA kwa niaba ya Irene Isaka, mkurugenzi wa mamlaka hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kujenga uelewa wa miongozo ya utekelezaji wa mifuko kwa mameneja na watendaji wa mifuko hiyo.

Msika amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama wakidai uandikishwaji umekuwa na kasoro hivyo SSRA imeamua kuhakikisha wanachama wanakuwa na uhuru wa kuchagua mifuko watakayo kwa mujibu wa sheria ya mamlaka sura ya 135 toleo la 2015 kifungu cha 30 inavyoelekeza.

“Mtakubaliana na mimi kwamba, uandikishaji wa wanachama ni moja ya jukumu la msingi la mifuko ya hifadhi ya jamii, shughuli za mifuko hii hutegemea michango ya wanachama, hivyo lazima watendaji wa mifuko hii muwe na uelewa na mzuri kuhusu kanuni na taratibu za uandikishaji,” amesema Msika.

Amesema kuwa, lengo la kuwepo kwa mamlaka hiyo ni kusimamia sekta ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, kulinda na kutetea maslahi ya wanachama.
Na kwamba, ni wajibu wa mifuko hiyo kufuata sheria, kanuni na miongozo ili kuboresha mafao na kuifanya iwe endelevu.

Onorius Njole, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria SSRA amesema kuwa, sheria na miongozo iliyopo sasa hairuhusu mwanachama kuhama mfuko mmoja kwenda mwingine bali anaweza kubadilisha kazi huku akiendelea kuchangia katika mfuko mmoja.

“Zamani mfanyakazi akibadilisha kazi analazimika kuhama mfuko jambo ambalo lilisababisha wafanyakazi wanapostaafu kupata mafao kidogo tofauti na muda aliofanyakazi,” amesema Njole.

Hivyo Njole aliwataka wafanyakazi kutafakari kwa kina kabla ya kuchagua mifuko watakayochangia ili kuepuka usumbufu huku akitoa wito kwa waajiri wote hapa nchini kuwasilisha mapema michango ya wanachama kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

error: Content is protected !!