May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai: Mama Samia hatabiriki

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Spread the love

 

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania, amewataka wateule wa Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, kuchapa kazi kwani kiongozi huyo hatabiriki. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Spika Ndugai ametoa ushauri huo leo Alhamisi tarehe 1 Aprili 2021, Ikulu ya Chwamwino jijini Dodoma, wakati anazungumzia hatua ya Rais Samia kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.

Jana Jumatano, tarehe 31 Machi 2021, Rais Samia alifanya mabadiliko hayo kwa kuwahamisha na kuteua mawaziri nane na manaibu waziri. Pamoja na kumteua Balozi Hussein Kattanga, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Akizungumza katika hafla ya uapisho wa viongozi hao iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma, Spika Ndugai amewashauri wafuate sheria na taratibu za kazi zao, ili wakwepe kuondolewa katika nyadhifa zao.

“Nataka kuwaibia siri, mama hatabiriki. Hivi leo hatujui kama tutatoka salama, kwa hiyo kama hatabiriki chapeni kazi fuateni sheria na taratibu za kazi,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema, hata jana hakuna mtu aliyejua kama Rais Samia atafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, bali walijua kiongozi huyo ataishia kumuapisha Dk. Phillip Mpango, aliyemteua kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

“Ndugu zangu waheshimiwa, jana tulikuja hapa kwa suala la uapisho wa makamu wa rais, lakini hafla mheshimiwa rais akatoka kivingine, rais tuliondoka hapa watu wamepita njia wanzojua wenyewe,” amesema Spika Ndugai.

Rais Samia amefanya mabadiliko hayo baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021.

Dk. Magufuli alifariki dunia kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam. Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

error: Content is protected !!