December 4, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai amedanganya

Job Ndugai, Spika wa Bunge akiendesha vikao. picha ndogo Mbunge Juliana Shoza akichangia bungeni

Spread the love

Na Mwandishi Wetu

SPIKA wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, aweza kuwa hajasema ukweli kuhusu madai kuwa hamfahamu na wala hajawahi kumuona zaidi ya mara mbili, mbunge wa Viti Maalum (CCM), Juliana Shonza.

Akizungumza kwenye mkutano uliopita wa Bunge mjini Dodoma, Spika Ndugai alisema hamfahamu Shonza na kwamba kwa maisha yake yote, amekutana naye mara mbili tu.

“…huyo mbunge anayetajwa huyo, Juliana Shonza, simfahamu. Nimekutana naye mara mbili tu kwenye maisha yangu. Simfahamu,” alisema Spika Ndugai.

Ndugai alikuwa akijibu madai yaliyotolewa na mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa kilichosababisha Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kupelekwa Polisi na kushitakiwa mahakamani, ni “ugomvi wa kimapenzi.”

Kubenea ambaye kama Lema, ni mbunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameshitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, akituhumiwa kumshambulia kimwili Shonza ambaye naye ni Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Shonza amepata ubunge akiwa mmoja wa wanachama walioingia CCM baada ya kufukuzwa uanachama Chadema kwa tuhuma za usaliti. Ijumaa ya wiki iliyopita, aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa naibu waziri katika mabadiliko ya pili aliyoyafanya kwa baraza la mawaziri aliloliunda Desemba mwaka 2015.

Mabadiliko ya kwanza yaliyokuwa madogo zaidi, aliyafanya Machi mwaka huu alipoteua mawaziri wawili: Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, badala ya Dk. Harisson Mwakyembe aliyemhamishia wizara ya habari.

Lema alimtuhumu spika kutokana na hatua yake ya kuagiza Kubenea akamatwe kokote aliko na kupelekwa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge.

Ndugai alisema, “…kwanza, Lema amemshutumu spika kwa sababu gani Kubenea aliitwa kwenye Kamati ya Ulinzi ya Bunge. Nahisi ni kwa sababu hayupo pamoja nasi. Ni mmoja wa wabunge, sipendi kumuita mtoro, lakini hajakuwapo pamoja nasi. Ndio maana baadhi ya mambo yamempita kidogo.

“Ninyi wabunge ndio mlioamua hapa, kwamba haya mambo yanayohusiana na usalama, yaende kwenye Kamati ya Ulinzi inayoongozwa na Mheshimiwa Adadi Rajabu… ndio mlioamua baada ya mambo yaliyompata Mheshimiwa Tundu Lissu.

“Haya mambo anayosema Kubenea yapelekwe huko. Ili hayo mambo anayoyasema barabarani, yapelekwe kwenye Kamati ili yaingizwe kwenye Kamati. Na hili kwa kila mtu ambaye ana habari.”

Hata hivyo, Bunge halijaweza kumsikiliza Anthony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), aliyekuwa wa kwanza katika wabunge wote, kufikanyumbani kwa Lissu, baada ya shambulio.

Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa kupigwa risasi mfululizo zipatazo 40 mchana wa Septemba 7 mwaka huu.

Alikutwa na kadhia hiyo alipokuwa amefika tu nyumbani kwake eneo la Area D, mjini Dodoma, akitokea bungeni alikokuwa anaendelea kuhudhuria vikao vya Bunge. Kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi, Kenya.

Komu amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba Lissu alifyatuliwa risasi 38. Pembeni mwa nyumba yake, pameokotwa maganda 38 ya risasi. Katika mlango wa kushoto wa gari alimokuwa wakati akishambuliwa, kumekutwa matundu 26 ya risasi; ni yeye (Komu) aliyekabidhi Polisi maganda hayo ya risasi.

Katika taarifa yake, Komu alisema: “kwenye dirisha la mlango wake, kuna matundu mawili na mlango wa abiria upande wa kushoto mwa dereva kumekutwa matundu 26. Nyuma kuna matundu manne.”

Akizungumzia madai kuwa Kubenea anasakamwa kutokana na wivu wa kimapenzi, Spika Ndugai anasema, “mimi sifahamu kama Kubenea anafamilia. Lakini nahisi ana familia. Kwa hiyo, sitaki kuuendeleza mjadala huu.”

Alisema, “huyo mbunge anayetajwa Juliana Shonza, ambaye katika maisha yangu mimi, nimewahi kumuona mara mbili tu. Nimemuona siku ambayo nimemuapisha na siku ambayo alikuja ofisini kwangu akilia kwamba amepigwa. Sijawahi kumuona tena.”

Ndipo akasema, “hata hapa bungeni sijui Shonza anakaa wapi. Ndio sijui. Kwa jina la Mungu, sijui, maana hata swali la nyongeza sijawahi kumpa (au hajamruhusu aulize).”

Juu ya maelezo yote hayo ya Spika Ndugai, yanayojikita kuwa hamfahamu mbunge Shonza, MwanaHalisi Online limebaini kuwa Juni mwaka huu, wakati bunge likijadili suala la kadhia ya wabunge Halima Mdee wa jimbo la Kawe Dar es Salaam, na Esther Bulaya wa Bunda Mjini mkoani Mara, alikuwa Shonza aliyewasilisha mapendekezo ya adhabu dhidi yao kuongezewa.

Kwenye kiti cha kuongoza majadiliano, alikuwapo Spika mwenyewe Ndugai. Ndio kusema kuwa aliyesimamia adhabu ya kufungiwa kwa wabunge hao wawili, ni Ndugai.

Mbunge kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambaye ameshurutisha kutotajwa kwa jina katika habari hii, amenukuliwa kupitia MwanaHalisi Onlineakisema: “Hata mapendekezo ya kuongeza adhabu kwa wabunge hao wawili, yaliingizwa bungeni kwa mamlaka ya Spika mwenyewe. Haiwezekani kuwa hamfahamu (Shonza).”

error: Content is protected !!