JOB Ndugai, Spika wa Bunge amezitaka Asasi za Kiraia nchini (AZAKI) kufanya shughuli zao walizosajiliwa na kuachana na masuala ya siasa, kwani wenyewe ni wanasiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo jana tarehe 8 Novemba 2019, katika hafla ya kufunga wiki ya AZAKI, iliyofanyika jijini Dodoma.
Aidha, Spika Ndugai amezitoa hofu AZAKI kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kwamba utafanyika kwa amani na utulivu.
“Muendelee kuwa na amani na utulivu, msiwe na wasiwasi tunapoelekea kwenye uchaguzi huo mkuu. Mengine ya wanasiasa mtuachie wenyewe, na wale mnaotaka kuingia kwenye siasa karibuni sana,” amesema Spika Ndugai.
Wakati huo huo, Spika Ndugai amezishukuru AZAKI kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa serikali na kwake pia.
“Wana AZAKI mwakani ni mwaka wa uchaguzi uchaguzi mkuu wa nchi yetu , ambako kutakuwa na uchaguzi wa madiwani, wabunge, lakini pia naamini rais wetu (John Magufuli) ataendelea. Sina hakika kama nitapata nafasi ya kukutana nanyi, kama mtaendelea kufanya maazimisho katika mwezi kama huu,” amesema Spika Ndugai na kuongeza;
“Maana wakati huo tutakuwa kwenye harakati kubwa sana, tarehe kama hizi uchaguzi mkuu ndio unakuwa ushafanyika, wanaokata rufaa wanakimbilia mahakamani, bunge linaundwa anapatikana spika mpya, baraza jipya la mawaziri, kwa mazingira hayo niwashukuruni sana kwa jinsi ambavyo mmenipa ushirikiano.”
Leave a comment