June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai awashukia wapinga tozo miamala ya simu

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewataka watu wanaopinga tozo ya miamala ya simu, waeleze njia mbadala itakayowezesha Serikali kupata fedha za kuwaletea maendeleo wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kiongozi huyo wa Bunge, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 23 Julai 2021, akizungumza katika kikao kazi cha Mkoa wa Dodoma, kilichoandaliwa na mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka.

Spika Ndugai amesema, Bunge lilipitisha sheria ya tozo hiyo, ili Serikali ipate fedha za kuibadilisha Tanzania kimaendeleo.

“…wewe unayepinga tozo hii, tupe njia mbadala tutapata wapi fedha. Maamuzi haya tumeyapitisha kwa nia njema kabisa, tuwe na Taifa ambalo ni tofauti,” amesema Spika Ndugai.

Tozo hizo zinazotozwa katika miamala ya simu, zilianza kutumika kuanzia tarehe 15 Julai 2021.

Ambapo Serikali inatoza kuanzia Sh. 10 hadi 10,000, katika muamala wa kutuma au kutoa pesa, kulingana na thamani ya muamala wa fedha husika.

Kupitia tozo hiyo, Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya Sh. 600 bilioni, katika mwaka wa fedha wa 2021/22, ambazo zitatumika katika kuimarisha huduma za afya, miundombinu ya barabara na elimu.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Spika Ndugai amesema, fedha hizo zitapelekwa katika mfuko maalumu wa Serikali, ulioanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.

“Bunge tulikaa kwa pamoja na kujadiliana, tukaamua kuwa na tozo kwenye miamala ya simu ili fedha zitakazopatikana zitaenda katika mfuko maalumu utakaowasaidia wananchi,” amesema Spika Ndugai.

Kauli hiyo ya Spika Ndugai anaitoa kipindi ambacho tayari Rais Samia Suluhu Hassan, amemwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kupitia malalamiko ya wananchi.

Tangu kuanza kutumika kwa makato hayo, malalamiko yamekuwa yakitolewa kuwa “yanawanyonya wananchi” hivyo yapunguzwe au yafutwe ili kuwaletea unafuu wananchi hao.

Kwa mujibu wa Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu, fedha zitakazopatikana kupitia tozo hiyo, zitajenga vyumba vya madarasa 10,806, vya shule za msingi na sekondari.

Pia, zitajenga shule za sekondari za kata 300 na shule za sekondari za sayansi za wasichana 10. Kwenye afya, fedha hizo zitajenga na kukamilisha zahanati 756 zahanati.

Kwenye miundombinu, fedha hizo zitajenga barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 250, kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa changarawe, urefu wa kilomita 5,834 na madaraja makubwa 64.

error: Content is protected !!