May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai awapa masharti wabunge

Waziri Mkuu akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewataka wabunge kuacha ngonjera katika kipindi cha maswali na majibu, ili kuokoa muda. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).

Spika Ndugai ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 24 Mei 2021, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.

“Naomba tujielekeze kwenye lengo la kikanuni la muda huu, nao ni kwamba unatakiwa uulize swali, habari ya kujenga hoja, kuzunguka, kufanya hivi ni kutupotozea muda. Mawaziri mjibu maswali msizunguke, jibu moja kwa moja. Kinachotakiwa ni jawabu,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema kuanzia kesho tarehe 25 Mei 2021, mbunge atakayekwenda kinyume na muongozo huo, atamkalisha chini.

“Ningeomba sana kuanzia kesho, baada ya kutoa muongozo huu wote tujielekeze hivyo. Unayesimama uliza swali vinginevyo tutakukalisha chini, tukikukalisha chini ni aibu kwa wapiga kura wako, haipendezi,” amesema Spika Ndugai.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Spika Ndugai amesema, kama wabunge watashindwa kutekeleza muongozo huo, mhimili huo utashindwa kumaliza maswali yaliyopangwa kuwasilishwa bungeni , katika vikao vya bajeti.

“Kabla hatujaanza maswali nitoe muongozo tena, sababu mnazidi kuwa wazoefu. Katika kipindi cha maswali kwenye bajeti ni saa moja tu, maswali yote 10 ni ngumu kuyamaliza, hatuwezi ku-run(endesha) kwa utaratibu huo.

Lakini tutajitahidi sana, twende kwa muda huo uliopangwa, ili ratiba nyingine ziende kama ilivyopangwa. ,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amewashauri wabunge, kuiga mfano wa vikao vya bunge vya nchi jirani, ambapo amesema wabunge wake huuliza maswali moja kwa moja.

“Tuwe tunaangalia mabunge ya wenzetu katika kipindi cha maswali na majibu , wanaenda swali, jibu. Swali, jibu ndiyo lengo lake katika kipindi hiki,” amesema Spika Ndugai.

error: Content is protected !!