April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai awanyoosha wapinzani bungeni, akiilinda mahakama

Job Ndugai, Spika wa Bunge la 12 la Tanzania

Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge, amezuia Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria kusomwa bungeni jijini Dodoma, kwa maelezo kwamba inashambulia Mhimili wa Mahakama. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hotuba hiyo ilitakiwa kusomwa bungeni hapo, jana tarehe 17 Aprili 2020, katika mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi, ya wizara ya katiba na sheria kwa mwaka wa fedha wa 2020/21.

Spika Ndugai amedai kuwa, hotuba hiyo imeandikwa kwa kutumia lugha inayotweza mhimili wa mahakama.

“Kubwa zaidi linalonisumbua, tumesisitiza si vizuri mhimili wa bunge kuwa kituo cha kushambulia mahakama. Kuanzia kifungu cha 66, 67, 68, 69, 70, 71, 72 na 74. Kila pahali pamekuwa na lugha ambayo ni ya kutweza mahakama. Kuonesha Mahakama ya Tanzania si chochote haipendezi,” ameeleza Spika Ndugai.

Sababu nyingine aliyotoa Spika Ndugai iliyopelekea kuzuia hotuba hiyo kusomwa bungeni, ni kutojikita katika mjadala wa upitishwaji wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, kwa mwaka ujao wa fedha.

“Tuanze kwanza ni nini madhumuni ya ya kikao hiki, madhumuni ni waziri wa katiba na sheria amewasilisha hoja mbele yetu. Bunge likubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya katiba na sheria, kwa mwaka wa fedha wa 2020/21. Hotuba hii kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho haijagusa bajeti hii,” amesema Spika Ndugai na kuongeza:

“Hakuna mahali inaonyesha bajeti hii.  Inaonekana kama imeandikwa na watu fulani mahali ambao hawajui nini kinaendelea bungeni.”

Aidha, Spika Ndugai amesema kama kambi hiyo haitarekebisha makosa hayo, hatosita kuzuia hotuba zake kusomwa bungeni.

Hii ni mara ya pili kwa Spika Ndugai kuzuia hotuba ya kambi rasmi ya upinzani kusomwa bungeni, ambapo mara ya kwanza alizuia hotuba kuhusu Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Bado meza ina shida na hotuba za kambi rasmi ya upinzani bungeni, na kama nilivyoanza na ofisi ya waziri mkuu, tusipotafuta namna ya kurekebisha hilo tatizo, basi itabidi twende hivyo hivyo maana mtakuwa mmechagua wenyewe,” amesisitiza Spika Ndugai.

error: Content is protected !!