SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge kuwa makini pindi wawapo majimboni kwao au nje ya jimbo kutokana na hali ya usalama kutokuwa shwari hapa nchini, anaandika Dany Tibason.
Ndugai alitoa rai hiyo kwa wabunge muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa kuahirisha Bunge mjini Dodoma.
Ndugai aliwataka wabunge hao kuwa makini muda wote na kwamba watakutana tena Dodoma Jumanne ya Novemba 7, mwaka huu.
Akitoa matangazo ya mwisho Ndugai amesema kutokana na kuwepo kwa hali tete ya usalama nchini wabunge pindi wawapo majimboni au nje ya majimbo ni vyema wakawa makini.
“Waheshimiwa wabunge mimi nichukue fursa ya pekee kuwapongeza kwa jinsi tulivyoendesha shughuli za kibunge na niwatakie safari njema huko muendako na tukutane hapa salama maana kalenda anayo yeye.
“Lakini ndugu zangu wabunge napenda kuwaambia kuwa ni vyema mkalinda usalama wenu, kulingana na hali ya usalama ilivyo sasa hapa nchini.
“Mmekuwa mkisikia matukio mbalimbali jinsi hali inavyokwenda hivyo ulinzi mtu anaanza nao yeye mwenyewe tusikae katika mabaa hadi saa sita usiku au kujiachia.
“Matukio ni mengi katika nchi yetu tutazame nyendo zetu na hata kama mtu ulikuwa umezoea kurudi nyumbani usiku sasa ni bora kubadilisha muda na angalau ukarudi mapema.
“Lakini pia ni wakati wa kuangalia usalama wa familia zetu nasikia watoto wanatekwa,wanauwawa na ni wakati mzuri kujua kuwa watoto wakienda shule wanaenda na nani wanakaa na nani na wanatunzwa na nani maana watoto wanapotea katika mazingira ambayo yanatatanisha.
“Wanaotulinada ni wachache sisi tuko wengi na wanatuongezea ulinzi tu hivyo ni jambo jema kuangalia maisha yetu na usalama wetu ili tuweze kufikia katika hali iliyo nzuri zaidi” amesema Spika.
Hata hivyo, Spika hakusita kurusha madongo kwa baadhi ya wabunge ambao wanatumia mitandao kumkosoa huku akisema kuwa hata wale ambao wapo wanatumia nafasi ya kumuuguza mgonjwa huku wakitukana waombewe kwa Mungu kwa maana hawajui watendalo.
Leave a comment