SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema, mwenendo wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, katika kutenga fedha za miradi ya maendeleo, kwamba ifikapo 2025 ‘itachukua na kuweka waah.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 22 Juni 2021, wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akifunga mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/22, bungeni jijini Dodoma.
Licha ya Spika Ndugai kutotaja tukio mahususi ambalo serikali hiyo inayoongozwa na Chama Cha Mpainduzi (CCM), itakwenda kuchukua na kuweka waah, 2025 Tanzania inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu.
“Kwa mtazamo huu naamini tukiendelea hivi katika miaka miwili mitatu inayokuja, 2025 basi tena. Ni kuchukua na kuweka waah, hakuna jambo lingine kabisa kabisa,” amesema Spika Ndugai.
Spika Ndugai amesema vyanzo vipya vya mapato vilivyomo katika bajeti ijayo, vitaiingizia mabilioni ya fedha Serikali, ambayo yatasaidia kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa mradi wa ufuaji umeme katika Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, kwenye Mto Rufiji na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR),.
Pia, Spika Ndugai amesema Serikali hiyo iliyoko chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuongeza fedha za utoaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Sababu pamoja na bajeti ile tuliyoipitisha, kwa maamuzi ya kodi, jinsi ambavyo nyongeza ya mabilioni ya fedha yanavyoenda katika maji, barabara, makazi, afya, mikopo ya wanafunzi elimu juu, masuala ya reli, bwawa la umeme, zile shida za wananchi ambazo wabunge tunahangaika nazo, haijapa kutokea, naipongeza Serikali,” amesema Spika Ndugai.
Mbunge huyo wa Kongwa (CCM), amesema uhitimishwaji mjadala wa bajeti hiyo haujawahi kutokea, hususani mapendekezo mapaya yaliyotolewa na Serikali kupitia tukio hilo.
“Miaka mingi kama mbunge, kweli kutoka moyoni mwangu sijawahi kuona Serikali ikija na uhitimishaji wa bajeti wa iana hii ya leo. Sisi kama wabunge tunapaswa kumpongeza rais wetu kwa mapendekezo haya yaliyokuja leo,” amesema Spika Ndugai.
Leave a comment