May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai ‘aota’ Katiba Mpya

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Spread the love

 

WAKATI wanasiasa, wanaharakati na wasomi wa kada mbalimbali nchini Tanzania, wakitaka mchakato wa Katiba Mpya uendelee, Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri, amehoji namna ya muundo wa Bunge litakalojadili Katiba Mpya siku zijazo, kwamba litakuwaje. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Akizungumzia namna ya kuiendea Katiba Mpya, Spika Ndugai amesema “…ni kuangalia kama (Bunge) moja linatosha au kuna haja ya kuwa na lingine dogo huko juu kama nchi nyingine zilivyo.”

Amesema, miongoni mwa mijadala itakayokuwepo katika mchakato huo, ni mabadiliko ya muundo wa mhimili huo.
Kiongozi huyo wa Bunge ametoa kauli hiyo leo Jumatano, tarehe 30 Juni 2021, akizungumzia maadhimisho ya siku ya mabunge duniani yanayofanyika tarehe 30 Juni kila mwaka.

Spika Ndugai amesema, mjadala huo utaangalia kama kuna haja ya kuwa na mabunge mawili au kubaki na moja.

“Leo ni siku ya mabunge duniani, niwaambie tu kidogo dondoo. Kuna mabunge 193 na katika nchi hizo 193, nchi 79 ikiwemo sisi tuna chemba moja ya mabunge na 114 kuna chemba mbili za mabunge. Bunge kama la kwetu na lingine dogo zaidi wengine wanaita seneti,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema, kwa ukanda wa Afrika Mashariki, nchi za Rwanda, Sudani Kusini, Burundi na Kenya zina chemba mbili za mabunge, huku Tanzania na Uganda zikiwa zina chemba moja.

Kwa sasa nchini Tanzania, wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu wameufufua upya mjadala wa mchakato wa Katiba Mpya, uliositishwa Aprili 2015, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa.

NEC ilisitisha hatua hiyo ya mwisho ya upatikanaji Katiba Mpya, kutokana na zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kutokamilika kwa sababu ya hitilafu zilizojitokeza katika mshine za BVR.

Tangu zoezi hilo kusitishwa chini ya aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, halikuendelea tena katika awamu zilizofuata.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, aliweka kando mchakato huo kwa maelezo kwamba alitaka kuijenga nchi.

Juzi Jumatatu, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa sababu zile zile alizowahi kutoa mtangulizi wake Dk. Magufuli kwamba, anaweka sawa uchumi wa nchi.

Kauli ya Rais Samia imechagiza baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kuanzisha upya vuguvugu la kudai Katiba Mpya.

Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), kesho Julai Mosi 2021, linatarajiwa kuzindua kampeni maalumu ya kudai katiba hiyo.

error: Content is protected !!