SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema, Halima Mdee na wenzake 18 waliofukuzwa uanachama Chadema “wataendelea kuwa wabunge halali labda wao wenyewe wapende kujiuzulu.” Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam …(endelea).
Ndugai ametoa msimamo huo leo Jumatatu ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kamati kuu ya Chadema tarehe 27 Novemba 2020 ilipoazimia kwa kauli moja kuwafukuza uanachama wa Chadema.
Mdee na wenzake 18, walituhumiwa kwa “usaliti, kughushi na uasi” wa chama hicho kwa kujipeleka kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Uamuzi wa kamati kuu, ulitolewa mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe tarehe 27 Novemba 2020 akisema, Mdee na wenzake wamekisaliti chama na kama hawaridhiki na uamuzi huo, wanaweza kukata rufaa baraza kuu ndani ya siku 30 au kuomba radhi.
Leo Jumatatu tarehe 30 Novemba 2020, Spika Ndugai mara baada ya kuwaapisha Humphrey Polepole na Riziki Lulida kuwa wabunge baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, amewajibu Chadema juu ya uamuzi wao.
Spika Ndugai amemtaka Mbowe kuacha kutumia mamlaka yake vibaya dhidi ya wanawake.
Amesema, Mdee na wenzake wamechukulia hatua ya kufukuzwa pasina kusikilizwa “Mbowe na (John) Mnyika (katibu mkuu wa Chadema) haiwezekani, wataendelea kuwa wabunge halali wa Bunge labda wao wenyewe wapende kujiuzulu.”
“Wabunge wote walioapishwa ikiwemo wale 20 wa Chadema, 19 na yule mmoja wa jimbo Aida Khenan ni wabunge halali. Niwahakikishe, wale 19 ni wabunge halali, labda wao wenyewe kwa mujibu wa Katiba yetu wapende wajiuzulu,” amesema Spika Ndugai.
Amesema, kama kulikuwa na tatizo kwa Mdee na wenzake 18 “wamekosea namna gani, tuwatafute, tuzungumze nao.”
Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa ni wale waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega.
Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga. Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao.Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.
Pia, Spika Ndugai ametumia fursa hiyo kuzungumzia mabadiliko ya kanuni za Bunge yaliyofanywa katika mkutano wa Bunge la 11 kuhusu uapishaji wa wabunge kuwa yalifanyika baada ya utafiti kubainisha mabadiliko ya kanuni ili kuondoa changamoto iliyokuwepo.
“Uapishaji wa wabunge nje ya Bunge ni jambo la kawaida. Sheria inatambua maeneo yote ya Bunge na spika anaweza kuelekeza wapi yafanyike,” amesema bila mabadiliko hayo, Mdee na wenzake 18 pamoja na Polepole na Riziki wangeapishwa 2 Februari 2021
“Shughuli za Bunge huwa hazisimamia na ndiyo maana wabunge wanachaguliwa kwa miaka mitano, mbunge haendi likizo, atakuwa jimboni, mikoani au kamati zetu za Bunge, kwa hiyo hakuna tatizo mtu kuapishiwa eneo lolote la Bunge,” amesema Spika Ndugai
“Kuna watu hivi karibuni, wamejipambanua na kukejeli shughuli za Bunge, niwatahadhalishe watu wanaodhalilisha Bunge, uongozi wa Bunge au wabunge waliokwisha kuapishwa. Tuzielewe kanuni za Bunge na utaratibu wake,” amesema Spika Ndugai
Leave a comment