Monday , 30 January 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Spika Ndugai amejaribu, ameshindwa
Makala & Uchambuzi

Spika Ndugai amejaribu, ameshindwa

Spika Job Ndugai
Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri amejaribu kumchora Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taswira hasi kwa Watanzania, lakini ameshindwa. Anaandika Bupe Mwakiteleko … (endelea).

Utafiti rahisi unaoweza kumsaidia msomaji ni kwamba, Spika Ndugai anapokutana na waandishi wa habari na kisha kusema kile anakusudia, mjadala unaoibuka hujielekeza katika kupinga kila sentesi yake.

Unapoangalia Televisheni za mtandaoni (TV Online) pale wanapoweka video ya kile alichozungumza, chini kabisa baada ya video zingine huwa kuna maoni ya watazamaji wa video hiyo (coments), ukipitia maoni hayo unapata jibu.

Taasisi za kiraia na zile za dini, zinamweka Spika Ndugai katika kundi la asiyeeleweka. Maandiko na video za viongozi wa dini zinazosambazwa, zinaakisi namna wasivyokubaliana na Spika Ndugai.

Narejea viongozi wawili wa dini tu kama mfano. Tazama andiko la Askofu Dk. BensonBagonza, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe kuhusu sakata la Spika Ndugai na Prof. Assad, anajielekeza katika kukinzana na mawazo ya spika.

Askofu Bagonza hakubaliani na hatua ya Bunge kumgomea Prof. Assad, hatua hiyo ilifikiwa baada ya kuibuliwa na kusimamiwa na Spika Ndugai. Mwisho Askofu Bagonza anashauri busara itumike.

Rejea video ya Sheikh Rajab Katimba, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania kuhusu sakata hili, Sheikh Rajab anakwenda mbali na kuhoji “….tatizo ni neno dhaifu ama kuna lingine?” hamweliewi Spika Ndugai.

Sheikh Katimba anasimamia hoja kwamba, hakuna mwanadamu asiye na udhaifu. Hapa alitaja ngazi mbalimbali ikiwemo spika, rais na CAG kwamba, wameumbwa na wanao udhaifu.

Yeye (Sheikh Katimba) haoni tatizo la uzito unaobebwa baada ya kuelezwa katika Bunge kuna dhaifu. Anashangazwa na Spika Ndugai anayedhani kutumika kwa neno hilo kwamba si sahihi.

Viongozi hawa wanabeba mfano wa viongozi wengine wanaoheshimika katika nafasi zao kwenye jamii. Wametoa maoni yao kama Watanzania, hawamwelewi Spika Ndugai, hasa msingi wa kile anachokisimia na umuhimu wa Ripoti ya Prof. Assad.

Taasisi za kiraia ikiwemo Change Tanzania ni mfano wa taasisi zinazoshangaa namna neno ‘dhaifu’ linavyomtaabisha Spika Ndugai.

Hawa wanatazama namna Ripoti ya CAG ilivyo muhimu kwa wabunge kuichambua kwa niaba ya wananchi.

Wanaangalia udogo wa mjadala wa neno ‘dhaifu’ halafu ukubwa wa ripoti hiyo ambayo haijadiliwa kwasababu tu neno ‘dhaifu’ lililotamkwa na Prof. Ndugai.

Kwa bahati mbaya ama nzuri, hakuna taasisi ama viongozi wa dini waliojitokeza na kumkingia kifua Spika Ndugai kwamba, yupo sawa katika mkasa wake na Prof. Assad. Waliojitokeza wanashindwa kumwelewa. Wanamshangaa.

Hapa anatajwa Spika Ndugai kwa kuwa, yeye ndiye aliyeibua mkasa huo, Bunge kwa kuwa lina wabunge wengi wa CCM wanaofuata milio ya zumari, likafanya uamuzi kwa ushawishi wa mtoa hoja.

Taasisi za kisiasa nazo zinamshangaa Spika Ndugai kwa kusimamia hoja hiyo. Maswali yanaibuka, nini kilicho nyuma ya pazia.

Viongozi wa dini, taasisi za siasa na za kiraia pia wananchi wanaotoa maoni kwenye mitandao ya kijamii wanasimama na Prof. Assad kwa kuwa tu, Spika Ndugai ameshindwa kujenga hoja inayowashawishi kuungaana naye.

Kheri James, Mwenyekiti wa UVCCM naye anashangazwa na namna Bunge linavyoweza kukwepa mjadala kuhusu Ripoti ya CAG kwa kuwa tu, kuna msuguano kati ya Prof. Assad na Spika Ndugai.

James anaona umuhimu wa Ripoti ya Prof. Assad zaid kuliko msuguano wa Prof. Assad na Spika Ndugai. Anasimama na uzalendo zaidi kuliko mvumo wa zumari.

Kinachostaajabisha zaidi ni kuwa, Spika Ndugai anadai kwamba, Yeye kwa mgongo wa Bunge hataki matumizi ya neno ‘dhaifu’ bila kujali uhalali wake katika lugha za kihesabu.

Zaidi ni pale anapokwenda mbali na kumshauri Prof. Assad ajiuzuli eti anampa tabu rais. Ninaamini kama Prof. Assad atachukua uamuzi wa kujiuzulu, atakuwa dhaifu kuliko namna inavyotarajiwa.

Mazungumzo na mijadala ya ana kwa ana mitandaoni, inajielekeza kumwelewa Prof. Assad zaidi kuliko Spika Ndugai. Laini pia mijadala hiyo inajielekeza kumuhitaji zaidi Prof. Assad kuliko Spika Ndugai.

Hoja inayojengwa hapo ni kuwa, Prof. Assad ni mtu imara, asiyetumikia tumbo kujenga hoja isipokuwa elimu na ujuzi wake.

Kwa maoni yangu, Tanzania inahitaji watu wenye Kariba ya Prof. Assad 1,000,000 kwa mustakabali wa nchi hii. Ni kwa kuwa, anajua thamani ya nafasi yake katika kuutumikia umma zaidi kuliko tumbo lake.

Ni kiongozi asiyetishika, bali anayefuata utaratibu uliokubalika na taifa, hana hulka ya kujipendekeza kama tulivyozoea, hajali cheo isipokuwa wajibu wake kwa Watanzania.

Kwa Prof. Assad wajibu kwanza cheo baadaye. Hongera Prof. Assad. Tunatamani viongozi wengi kama wewe, lakini kwa bahati mbaya hawapo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuMakala & UchambuziTangulizi

Shule ya msingi yajengwa miaka 25 bila kukamilika, wanakijiji wachoka kuchangia

Spread the love  Wakazi wa Kijiji cha Makomba kilichopo kata ya Makazi...

Makala & UchambuziTangulizi

Hawatatukana watafufua makaburi

Spread the love  VYAMA vya siasa nchini Tanzania vimefunguliwa kutoka katika kifungo...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Panda, shuka ya Diwani Athuman kabla na baada ya kung’olewa Ikulu

Spread the love  HUENDA tarehe 5 Januari 2023, ikawa ni siku chungu...

Makala & Uchambuzi

Kwa nini walemavu wasioona wanalilia kondomu za nukta nundu?

Spread the loveKWENYE moja ya vikao vya kamati ya watu wenye ulemavu...

error: Content is protected !!