January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai alipasua Taifa

Job Ndugai, mgombea Uspika akijinadi mbele ya wabunge

Spread the love

 

MJADALA kuhusu kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai,  iliyodai  iko siku nchi itapigwa mnada kutokana na kuelemewa na madeni, umezidi kushika kasi, huku ukiacha mgongano kwa viongozi wa kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Spika Ndugai alitoa kauli hiyo tarehe 27 Desemba 2021, akiwa jijini Dodoma, akikosoa hatua ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuchukua mkopo wa Sh. 1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Kwa ajili ya kukabilia na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVUKO-19), kupitia utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.

Tangu Spika Ndugai atoe kauli hiyo, umeibuka mjadala mkali juu ya hali ya deni la Taifa, ambapo baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanamuunga mkono, huku wa Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), wakitoa matamko hadharani ya kumpinga.

Leo Jumapili, tarehe 2 Januari 2022, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameukoleza moto mjadala huo, akishauri kauli ya Spika Ndugai isipuuzwe, bali ifanyiwe kazi kwa maslahi ya Taifa.

“Kukopa anakosema Spika Ndugai, iwe ni ametuamsha kutoka usingizini, tulichukulie chanya badala ya kulichukulia hasi.  Kumtukana tukana tu si sawa, tusimchukulie hasi. Akitamka vile spika anatamka mtu mzima,” amesema Mbatia.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, hatua ya Spika Ndugai kuikosoa  Serikali kwa kuendelea kukopa fedha katika taasisi za fedha za kimataifa, sio ya kubezwa kwani anatakeleza majukumu yake ya kuishauri Serikali.

“Unajua Spika  Ndugai wanamtukana tukana tu, kwanza mihimili ikigongana ndiyo kazi yake. Kwa mujibu wa katiba Bunge kazi yake ni  kuishauri Serikali, ametoa hoja yake tuko wapi leo na hoja yake ni kweli,” amesema Mbatia na kuongeza:

“Unajua  hii mambo sio ya chama kimoja kwamba  inatakiwa akamnon’goneze Rais,  kesho akiwa hayupo deni linalipwa na wananchi.  Inapotokea migongano kama hii, ni afya kwa taifa,  maneno yenye ukinzani ndiyo yanaleta afya zaidi.”

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi

Mbatia amefuata nyayo za Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, aliyeunga mkono kauli ya Spika Ndugai, akisema kiongozi huyo wa Bunge alikosea kusema iko siku nchi itapigwa mnada, akidai imeshapigwa mnada tayari.

Lissu alitoa kauli hiyo juzi tarehe 31 Desemba 2021, akitoa salamu zake za kuuaga mwaka huo. Alidai Serikali inakosea kukopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, isiyokuwa na tija kwa taifa.

Siku moja baada ya Spika Ndugai kutoa kauli hiyo, tarehe 28 Desemba 2021, Rais Samia akihutubia katika halfa ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), jijini Dar es Salaam, alisema Serikali yake itaendelea kukopa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo.

Baada ya Rais Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa,   kutoa kauli hiyo, viongozi kadhaa wa chama hicho, waliibuka hadharani na kumuunga mkono huku wakipinga kauli ya Spika Ndugai.

Miongoni mwa viongozi waliotoka hadharani kumpinga Spika Ndugai, ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Kenan Kihongosi. Wenyeviti wa CCM Mikoa, Dk. Anthony Diallo  (Mwanza) na Kate Kamba (Dar es Salaam).

error: Content is protected !!