March 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai alia na Zitto

Spread the love

ZITTO Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini ni mwanasiasa anayemsumbua Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa na spika mwenyewe leo tarehe 17 Januari 2019 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam na kwamba, sasa anatafuta ushauri wa jinsi ya kumshughulikia kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Spika Ndugai anamtuhumu Zitto kwamba anapotosha baadhi ya mambo mara kwa mara.

Mambo ambayo Spika Ndugai amedai kwamba, yanapotoshwa na Zitto ni pamoja na sakata la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa mbele ya Kamati ya Maadili tarehe 21 Januari 2019.

Prof. Assad ameitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kwa madai ya kulidharau Bunge pale alivyofanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Kimataifa na kusema kuwa, Bunge lina udhaifu kutokana na kutotekeleza baadhi ya majukumu yake.

Akizungumzia sakata la Prof. Assad, Spika Ndugai amesema Zitto amedanganya watu kwamba, CAG ni mhimili wa nne hivyo haupaswi kuhojiwa na kamati hiyo. “Ukweli ni kwamba, CAG hawezi kuligomea Bunge,” amesema Spika Ndugai.

Pia, Spika Ndugai ameonekana kukerwa na namna Zitto anavyolibeba suala la Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kwamba, anaendeleza mkondo ule ule wa upotoshaji.

“Muswada wa Vyama vya Siasa uko kule unaendelea kama kawaida, sasa hivi upo kwenye ngazi ya kamati, tukianza Bunge muswada unaingia. Wao kama wanakimbia kimbia kwenye korido za Dar es Salaam muswada utatungwa,” amesema Ndugai.

Hata hivyo Spika Ndugai amedai kuwa, kinachomchochea Zitto kufanya upotoshaji ni kusaka umaarufu na kwamba, hivyo hawezi kumtoa bungeni kwa kuwa ni mbunge pekee anayewakilisha chama chake.

“Ni kweli Zitto Kabwe ananisumbua sana lakini ukisema umtoe bungeni unawaza mtu mwenyewe yuko peke yake, ukimsimamisha atawakilishwa na nani? Unamuacha tu ndio maana hata kesi hizo anafanya peke yake maana yuko mwenyewe,” Spika Ndugai.

error: Content is protected !!