December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai: Mbowe usijipime ubavu na rais

Spread the love

JOB Ndugai, Spika wa Bunge ameonesha kukerwa na kitendo cha Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Deemokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, kuzungumza na wanachi baada ya Rais John Magufuli kufanya hivyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Jana tarehe 17 Mei 2020, muda mchache baada ya Rais Magufuli kuzungumza na kuonesha matumaini ya kupungua kwa maambukizi ya virusi vya corona, Mbowe alizungumza na wananchi kupitia mitandao ya kijamii akionesha mashaka na matokeo ya virusi, endapo havitadhibitiwa.

Rais Magufuli alizungumza alipohudhuria ibada ya Jumapili, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Chato mkoani Geita.

“…na kwa trend (mwenendo) wiki inayoanza nimepanga kufungua vyuo ili wanafunzi wetu waendelee na masomo, nimepanga pia sisi kama taifa michezo iendelee kwa sababu michezo ni sehemu ya burudani kwa Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Mbowe alipozungumza alisema “….janga hili halihitaji masihara, halihitaji mdhaha wala halihitaji usiri katika kulikabili.

Tulishauri sana serikali kuacha kuficha au kupunguza idadi ya waathirika na hatimaye vifo, tukiamini ukweli na ukubwa wa janga hili kujulikana kutaongeza ufahamu wetu na umakini.”

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma leo tarehe 18 Mei 2020, Spika Ndugai amesema, kilichofanywa na Mbowe kinaonesha kujipima ubavu na mkuu wa nchi (Rais Magufuli).

“Kama Mbunge wangu nimshauri, kuzungumza baada ya kiongozi wa nchi kuzungumza na Taifa, na kuanza kuzodoa kile ambacho amekizungumza ni kujipima ubavu na mkuu wa nchi. Ningemshauri sana  Mbowe aache tabia hiyo, ni tabia mbaya,” amesema Spika Ndugai huku akifafanisha kitendo chake ni sawa na kumzodoa Rais Magufuli.

Spika Ndugai amesema, mahali ambapo Mbowe alipaswa kuzungumza ma kutoa ushauri ni bungeni na si mitaani.

“Kiongozi ni kiongozi, rais ni kiongozi mkuu wa nchi hii, na Watanzania na yeye (Mbowe). Ni hekima kubwa kumheshimu na kumpa nafasi kuiongoza nchi.

“… na yeye (Mbowe) atumie nafasi yake kushauri inapobidi na mahali husika. Na mahala pake kwa kushauri ni bungeni na si mitaani anavyofanya,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge na Mbunge wa Kongwa, Dodoma amemtaka Mbowe kufanya kazi na Rais Magufuli, ikiwa ni pamoja na kuwa mzalendo na nchi yake.

“Nimshauri kujitahidi kufanya kazi na rais, Freeman ukimdharau rais umetudharau sisi wote, hauwezi kufanya kazi na sisi.  Ni vigumu, yule ndio mkuu wa nchi.  Jiepushe njia unazoendea hazikusaidii,” amesema Spika Ndugai.

Akizungumzia madai ya Mbowe ya kwamba Bunge halitekelezi wajibu wake inavyostahili, Spika Ndugai amedai kwamba, mwanasiasa huyo anapitwa na mambo mengi yanayotokea bungeni kutokana na utoro.

“Nisikitike kusema ni mtoro sana, na nyinyi ni mashidi anapenda kufanya vitu nje ya box, anapitwa na mambo mengi, akitoka nje anashutumu anamshutumu spika,” amesema Spika.

Hata hivyo, amemtaka Mbowe kurejesha Sh. 2,040,000 za bunge ambazo ni za posho za vikao vya Bunge ambavyo hajahudhuria.

“Ukichukua pesa hakikisha unarudisha mahali pake, ndio maana nikawataka warudishe milioni 110 za wananchi, sasa sijui hapo spika amekosa nini? Maana ni taratibu tumejiwekea wenyewe. Mil 2, 040,000 lazima arudishe, ni taratibu za kifedha,” amesema na kuongeza:

“Kitendo cha mpaka leo kutorudisha fedha, kinaonesha alikuwa ana nia ovu ya kuzichukua. Arudishe fedha, kwa upande huo tutaonana wabaya bure.”

error: Content is protected !!