Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Akson, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuzindua makala maalumu ya kutangaza vivutio vya utalii nchini inayofahamika kama ‘Royal Tour’ jijini New York, nchini Marekani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Pongezi hizo zimetolewa leo Jumanne, tarehe 19 Aprili 2022, bungeni jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.
Spika Tulia amesema wabunge wametoa pongezi hizo, kwa kuwa Rais Samia ametekeleza kiu yao ya kuongeza idadi ya watalii.
“Tunatambua siku ya jana Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua makala maalumu ya kuhamasisha utalii Tanzania na kwa sababu wabunge huwa mnachangia kuhusu kuongeza idadi ya watalii wanaokuja, sisi kama Bunge tunampongeza Rais kwa hatua anazochukua kwenye hili eneo,” amesema Spika Tulia.
Aidha, Spika Tulia amewataka wabunge wafuatilie ziara ya Rais Samia nchini Marekani, ili waweze kujua namna ya kushauri kwa ajili ya uboreshaji wa suala hilo.
“Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii itakuja baadae, ni muhimu kila mbunge afuatilie mambo yanayoendelea huko ili kama kutakuwa na la kushauri hapa na pale, itakuwa rahisi zaidi. Baada ya kujua hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na zile mnazotamani ziongezeke,” amesema Spika Tulia na kuongeza:
“Baada ya hapo ni muhimu kufuatilia ziara hii ya Rais Marekani ya kutangaza Taifa letu Tanzania.”
Leave a comment