May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika ashangaa vijiji kukosa umeme

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ameshangazwa na kitendo cha Tarafa ya Mungaa, iliyoko katika Jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida, kuwa gizani kwa kukosa umeme. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Spika Ndugai alishangazwa na taarifa hiyo, leo tarehe 28 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma, baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu, kusimama bungeni na kusema vijiji vyote vya tarafa hiyo, havina umeme.

Miraji alisema“nahitaji nipate uhakika, kwa kuwa umeme ni chachu ya maendeleo na kwa kuwa ni asilimia 44 ya vijiji vya Singida Mashariki vina umeme. Hususan Tarafa ya Mungaa, ambayo ina kata saba haina umeme kabisa?”

“Lini mkandarasi atakwenda kuanza kazi, kama ilivyosema Machi mpaka na sasa hajapatikana. Tunataka tujue jina la mkandarasi yule,” alisema Mtaturu.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Baada ya Mtaturu kuuliza swali kwa Wizara ya Nishati, Spika alihoji akisema “yaani Mtaturu kuna tarafa ambayo haina umeme, tarafa nzima?”

“Ngoja nikae vizuri, majibu naibu waziri kwa swali hilo, yaani humtakii mema Mtaturu kabisa. Hebu tusikie majibu,” alisema Spika Ndugai.

Kufuatia kauli hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, alisema Serikali kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeshaanza kutatua changamoto hiyo.

“Tunakiri kweli kuna baadhi ya vijiji Tanzania havijafikiwa na umeme, kama tulivyosema tulianza tukiwa na vijiji 12,268. Lakini tumepunguza mpaka sasa tuna vijiji 1,974, havina umeme na mpango uliopo ni kuhakikisha kabla Desemba 2022, vijiji vyote vinapata umeme,” alisema Byabato.

Byabato alisema, tayari wizara imemuagiza mkandarasi wa mradi huo mkoani Singida, Kampuni ya Sengerema, aende mkoani humo kabla ya Jumatatu tarehe 31 Mei 2021. Kuanza kazi ya kusambaza umeme katika tarafa hiyo na vijiji vingine vya Singida Mashariki.

Dk. Medard Kalemani, Waziri wa Nishati

“Katika eneo hilo ambalo Mtaturu ametaja, kazi inaendelea na tutafikisha umeme katika maeneo hayo. Tunatarajia hadi Disemba 2021, mkandarasi atakuwa amemaliza kupeleka umeme katika vitongoji vyote,” alisema Byabato.

Licha ya maelezo ya naibu waziri huyo, Spika Ndugai alimsimamisha Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ili atoe kauli ya msisitizo kuhusu uatuzi wa changamoto hiyo.

“Waziri, Mtaturu angekusikia tu kidogo ingemfariji. Pamoja na majibu mazuri ya naibu waziri,” alisema Spika Ndugai.

Akijibu swali hilo, Dk. Kalemani alisema tayari mkandarasi amekwenda mkoani Singida, kwa ajili ya kuanza kazi, ambayo itakamilika ndani ya miezi 18, kuanzia jana tarehe 27 Mei mwaka huu.

“Ni kweli jimbo la Mtaturu kimsingi ile tarafa ambayo haijapata umeme, wakandarasi wameondoka jana kwenda Singida kufanya kazi.

Pamoja na tarafa hiyo, Mtaturu alikuwa na vijiji 12 havijaguswa kabisa. Niwahakikishie wote watapata umeme ndani ya miezi 18 kuanzia jana walipoondoka wakandarasi,” alisema Dk. Kalemani.

error: Content is protected !!