Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Spika ampa onyo Waitara, ampiga dongo
Habari za SiasaTangulizi

Spika ampa onyo Waitara, ampiga dongo

Mwita Waitara
Spread the love

 

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amemuonya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM) baada ya kubeza na kupinga maelekezo aliyoyatoa kwa Serikali kwamba ndani ya siku 90 ichunguze malalamiko yaliyotolewa na wabunge dhidi ya mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali.

Pia amesema kwa maelezo aliyokuwa ameyatoa kwa Serikali yalijitosheleza kiasi kwamba mtu yeyote mwenye akili zake timamu, mtu mzima mwenye afya ya akili alipaswa kuelewa maana ya maelezo hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Spika Tulia ametoa kauli hiyo leo tarehe 14 Juni, 2022 bungeni jijini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu ambapo alianza kwa kuwaelezea wabunge namna alivyotoa maelezo kuhusu malalamiko ya Waitara.

Tarehe 3 Juni, mwaka huu, Waitara na Mbunge wa Songwe, Philip Mulugo wakati wakichangia makadirio ya bajeti ya wizara ya maliasili na utalii, walidai kuna mauaji yanayotokana na wanyama pamoja na walinzi wa hifadhi ya Serengeti.

Waitara alitaja majina ya 14 ya watu katika jimbo lake ambao amedai kuwa waliuawa ama kupotea akiwatuhumu wahifadhi katika hifadhi ya Serengeti kwamba wamekuwa chanzo cha matukio hayo wakati Mulugo alidai watu 80 wameuawa kwa kuliwa na wanyama na wengine kujeruhiwa na kubaki na ulemavu wa kudumu.

Kutokana na tuhuma hizo Spika Tulia alitoa siku tano kwa wabunge hao kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo bungeni ambapo tarehe 9 Juni mwaka huu, Kiongozi huyo wa Bunge alitoa maelezo ya kina bungeni na kuongeza kuwa wabunge hao wameshindwa kutoa udhibitisho wa tuhuma walizotoa.

Spika Tulia alitoa siku 90 kwa Serikali kuchunguza malalamiko hayo kisha kuwasilisha taarifa bungeni.

Aidha, akifafanua sakata hilo kwa wabunge leo, Spika Tulia amesema Waitara amekiuka kanuni za Bunge baada ya kwenda kwenye vyombo vya habari kupinga na kubeza uamuzi huo wa kiongozi wa Bunge.

“Kwa kuzingatia manufaa ya uamuzi huo, Nilitegemea mbunge husika Waitara angeshukuru badala ya kubeza na kupinga.

“Siku moja baada ya uamuzi wangu, nimesoma makala inayopinga na kuhoji juu ya uhalali na uamuzi wa maelekezo niliyoyatoa.

“Makala hiyo imeandikwa katika gazeti la Raia mwema la tarehe 10 Juni, 2022 ilitambulishwa kwa wino mweusi katika ukurasa wa mbele ‘Waitara apinga uamuzi wa Spika’, amesema.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson

Amesema habari hiyo ilimnukuu Waitara kwamba; “Ni vigumu serikali inayotuhumiwa kutenda jambo fulani, kwenda kujichunguza na badala yake bunge lilipaswa kuunda kamati teule kuchunguza na taarifa kuwasilishwa kwake si kama alivyofanya Spika.

“Hifadhi ya Serengeti ni ya serikali, sasa serikali inawezaje kujichunguza, kwa kuwa serikali inalalamikiwa na Spika amewahi kuwa Naibu Mwanasheria mkuu wa serikali ilipaswa ilitakiwa iundwe kama teule ya bunge iende ikachunguze kisha taarifa iwasilishwe bungeni.

“Ripoti ikija bungeni ijadiliwe na maazimio au mapendekezo yawasilishwe serikali, sasa swereikali kwenda kujichunguza kuna shida.”

Kutokana na nukuu hiyo ya Waitara, Spika Tulia amesema kauli ya mbunge hiyo inataka kuna shida serikali kwenda kujichunguza.

“Ina maanisha kuwa serikali na vyombo vyake vyote vya uchunguzi, kama vile polisi, Takukuru, Jeshi usu, usalama navyo vina shida, jambo ambalo si kweli,” amesema.

Amesema kwa kwa kuwa jambo hilo alishalitolea uamuzi, kitendo cha Waitara kuupinga kwenye chombo cha habari kinaenda kinyume na kanuni na taratibu za uendeshaji wa Bunge ambazo zinaweka wazi ni nini mbunge anapaswa kufanya anapoona hajaridhishwa na uamuzi wa Spika.

“Kanuni ya 5(4) inaweka wazi mbunge ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika anapaswa kuwasilisha malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge kwa maandishi, ili malalamiko hayo yafanyiwe kazi kwa mujibu wa kanuni.

“Waitara hakutaka kutumia utaratibu huo wa kikanuni na badala yake akaamua kwenda kulalamika kwenye vyombo vya habari na maelezo ya Waitara dhidi ya uamuzi wangu, yanakiuka sheria na kanuni zetu,” amesema.

Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 24 (e) cha sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge sura ya 296, inazuia mbunge au mtu yeyote kutoa maneno yanayovunja heshima ya Spika na kudhalilisha makusudi mwenendo wa shughuli za Bunge.

Amesema makosa aliyoyafanya Waitara yanaangukia katika kanuni ya 84 (1),(a) na (j) ambayo inasimamia na kutoa adhabu juu ya utovu mkubwa wa nidhamu.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni hiyo makosa ya Waitara yanajidhihirisha kuwa amepuuza uamuzi au maelekezo ya Spika aliyoyatoa kuhusu kuipelekea serikali tuhuma zilizotolewa ili ifanye uchunguzi na baadaye ikuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo bungeni.

“Kitendo cha kueleza kuwa Spika amewahi kuwa Naibu Mwanasheria mkuu wa Serikali kina lengo la kushusha hadhi ya Spika wa Bunge, kwa ujumla kwamba bunge linaongozwa na Spika ambaye anafahamu sheria lakini hafuati sheria.

“Ninyi nyote mnafahamu na yeye pia anafahamu kuwa kusema mimi niliwahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali anapaswa ajue najua utaratibu kuliko yeye. Kwa hiyo hilo tu kwa kuwa analijua alipaswa ajue kwamba hawezi kuwa yeye anazijua sheria kuliko mimi.

“Kwa sababu hiyo siku tarehe 9 Juni, nilitoa maelezo kwa kirefu sana hapa. Mtu yeyote mwenye akili zake timamu, mtu mzima mwenye afya ya akili alipaswa kuelewa maana ya yale maelezo niliyoyatoa wakati ule,” amesema.

Amesema kwa mamlaka aliyonayo anaweza kutumia kanuni 84 inayozungumzia adhabu anayotakiwa kupewa mbunge kwa utovu mkubwa wa nidhamu.

“Pamoja na uzito wa hiki kitendo alichokifanya Waitara ambaye si mbunge mpya. Nampa onyo asirudie kudharau maamuzi ya Spika na kwa sababu kanuni hiyo adhabu zake ni nzito, lakini baada ya kumpa onyo hilo nimemsamehe,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!