July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Soko lajengwa kwa miaka 13

Spread the love

SOKO la Buigiri lililopo katika Wilaya ya Chamwino, Dodoma limeanza kujengwa tangu mwaka 2003 na halijakamilika, anaandika Dany Tibason.

Seleman Jafo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ameupa mwezi mmoja uongozi wa Halmashauri ya Chamwino ili kuhakikisha soko hilo linafanya kazi.

Ametoa gizo hilo jana baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani hapo na kubaini kuwa, soko hilo halifanyi kazi kwa miaka 13 sasa.

Amesema kama watashindwa kutekeleza Ofisa Masoko, Biashara na Uwekezaji wa halmashauri hiyo vibarua vyao vitakuwa hatarini.

Jafo amesema, inashangaza kuona majengo ya soko hilo yakiendelea kuwa magofu wakati yangeweza kufanya kazi kama soko la zabibu na kuipatia mapato halmashauri hiyo.

“Unapoweka mradi sehemu yeyote lazima ufanye utafiti, sasa mmetengeneza soko hili kwa kutumia fedha za wafadhili lakini halitumiki kama ilivyotarajiwa na badala yake halmashauri inashindwa kulifanya kuwa chanzo cha mapato, wakati haijitoshelezi kimapato,” amesema Jafo.

Amebainisha kwamba wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya zenye mapato chini ya Sh. 500 milioni kwa mwaka kutokana na kutokuwa wabunifu kwenye vyanzo vya mapato.

“Makusanyo mliyonayo ni madogo mtajiendesha vipi kama hata soko mnalo lakini mnashindwa kuwa wabunifu ili liwe sehemu ya nyie kujiongezea mapato,” amehoji.

Yusuph Jirico, Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino amesema, jengo hilo lilianza kujengwa kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) mwaka 2003 ili kuwasaidia wananchi wanaolima mbogamboga kwenye skimu ya umwagiliaji ya Buigiri waweze kufanya biashara zao.

Keneth Yindi, Diwani wa Kata ya Buigiri amesema soko hilo lingetumika ipasavyo, lingeweza kuongeza kipato kwa watu wa Buigiri.

error: Content is protected !!