May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Soko la madini Mererani lawagawa wabunge

Joseph Kasheku 'Msukuma,' Mbunge wa Geita Vijijini

Spread the love

 

UHAMISHAJI soko la madini ya Tanzanite kutoka Arusha kwenda Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, limewagawa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mvutano huo umeibuka leo Ijumaa, tarehe 29 Aprili 2022, bungeni jijini Dodoma, baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, kuishauri Serikali irudishe soko la madini hayo jijini Arusha, akidai uhamishaji huo umeikosesha Serikali mapato.

Soko hilo la madini ya Tanzanite, lilihamishwa kutoka Arusha kwenda Mirerani, Julai 2021, baada ya Serikali kufanya marekebisho ya kanuni za biashara ya madini hayo kwenye Mgodi wa Mirerani.

“Dhana nzima ya kuondoa madini ya Tanzanite na kutaka yauzwe Mirerani peke yake inahusisha maeneo mawili, kwanza kudhibiti utoroshaji wa madini na pili kuujenga mji wetu wa Mirerani, hoja ambayo kila mtu anaikubali na sisi hatutaki yauweze Arusha peke take,” amesema Gambo na kuongeza:

“Lakini kuna changamoto tumepata kutokana na maamuzi ya Serikali, kwanza mapato yake yameshuka kutoka 1.3 bilioni yaliyokusanywa kabla ya uamuzi, ambapo Tanzanite peke yake ilikuwa Sh. 800 milioni, leo tumepeleka Mirerani tunapata Sh. 339 milioni. Kwa hiyo Serikali imepata hasara.”

Hoja hiyo ya Gambo iliungwa mkono na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye amesema uhamishaji wa soko hilo, kutoka Arusha kwenda Mirerani, itasababisha hasara ya uharibifu wa miundombinu ya soko la awali.

“Kwanza kabisa huyu mbunge ambaye amemaliza kusema (Gambo), nitumie dakika yangu moja kuwasaidia wanaopanga mambo ya madini. Tanzanite tulijaribu kuweka kituo kikubwa kiwe Arusha na tukaweka mitambo ya kuchonga na kuongeza thamani, ukisema madini yasiende Arusha, basi mitambo hiyo yote inakuwa imeharibika,” amesema Prof. Muhongo.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na wabunge kadhaa, akiwemo Mbunge Viti Maalumu kutoka mkoani Manyara, Regina Ndege, ambaye ameshauri soko hilo libaki mkoani humo kwa kuwa umekidhi vigezo.

“Nashauri soko la madini kubaki pale Mirerani, kwa nini tunasema libaki? Wakati tunagawanya limeendelea kubaki Manyara lakini waliangalia vigezo gani au shughuli gani za kiuchumi, mkoa wetu unabebwa na Tanzanite, shughuli za kilimo. Serikali waendelee kubakiza soko Mirerarni,” amesema Ndege.

Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini (CCM)

Aidha, Ndege ameiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa soko hilo ili lifanye kazi.

Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, ameunga mkono soko hilo libaki Manyara, akisema kitendo hicho kitaufanya mji huo kukuwa.

Kuhusu hoja ya soko hilo jipya kutokusanya mapato mengi ya madini hayo, Musukuma ameshauri viongozi wake waende mkoani Geita, wakajifunze namna ya kuongeza mapato.

“Tulivyopitisha sheria ya kurudisha masoko kwenye maeneo husika, sisi watu wa Geita ndiyo tuliileta 2018 na Bunge lako tukufu likatupitishia sheria. Sisi Geita ni wanufaika namba moja na watu wa Simanjiro ningeshauri wajifunze kwetu, tunakusanya sokoni karibia Sh. 3 bilioni,” amesema Musukuma na kuongeza:

“Arusha nisehemu ambayo ina utalii mwingi, tusionee wivu tuache miji midogo nayo ikue kwa kukusanya mapato.”

error: Content is protected !!