
DVD za filamu zikiuzwa mtaani
SOKO la Filamu nchini limetajwa kuangukia pua na kupoteza umaarufu kutokana na kukosekana kwa ubunifu katika kazi hizo pamoja na wizi wa kazi za wasanii uliokithiri. Anaandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).
Filamu zinazorekodiwa nchini zinadaiwa kupoteza umaarufu nchini kiasi cha kusababisha soko lake kuangukia pua, huku waandaji na wasambazaji wake wengi wakiamua kujitoa na kutafuta shughuli zingine za kufanya.
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa wasambazaji wa kazi za Sanaa nchini, ‘Tanzania Audio Visual Works Distributors,’ Baraka Nyanda, wamelaumu kushuka kwa ubunifu miongoni mwa wasanii.
Aidha,amesema kukosa ubunifu kumepelekea kuwepo wa sinema na miziki hafifu isiyoweza kustahimili ushindani wa soko la kazi za burudani duniani.
“Tathmini kutoka wasambazaji waliochini ya ‘Tanzania Audio Visual Works Distributors,’ ambao wanafikia 200 kwa sasa, imeonesha kupungua kwa kazi za Sanaa yaani muziki na filamu kwa asilimia Zaidi ya 50 na hii imesababishwa na kukosekana kwa masoko ya kazi hizo nchini,” amesema Nyanda.
Wakizungumza jijini hapa wakati wa kikao maalum kati ya wasambazaji na wasanii, viongozi hao wamebainisha kuwa tasnia ya filamu na muziki nchini ilikuwa na mafanikio kuanzia mwaka 2005.
Amesema zaidi ya kazi 300 zilikuwa zinafyatuliwa kila mwaka kwa mujibu wa ripoti ya Media for Development International ya 2011.
“Kipindi hicho tulishihudia filamu mpya takriban 10 zikitolewa kila wiki, lakini hali ni tofauti kwa sasa ambapo tunashuhudia chini ya filamu 10 kwa mwezi mzima huku idadi hiyo kwa mwaka ikiwa ni wastani au chini ya sinema 120 tu hii ni kwa mujibu wa rekodi ya wasambazaji wa kazi za Sanaa nchini kwa mwaka huu wa 2015,” amesema Nyanda .
“Wasambazaji na waandaaji (producers), wa sinema na muziki wameamua kujitoa kwenye tasnia hii na kutafuta shughuli mbadala za kufanya,” amesema.
Ameongeza kuwa wasanii wengi wa muziki wamekuwa wakisambaza kazi zao kupitia mitandao kama You-Tube ambako mashabiki wao huzichukua bure huku wengine huthubutu hata kugawa CD za nyimbo zao mpya bure kabisa mitaani.
Nae msanii wa filamu, Simon Mwapangala maarufu kama ‘Rado,’ amesema kuwa hata kampuni za usambazaji filamu zinachangia kuua tasnia hiyo kwa kuwapa waandaaji malipo finyu; “Hawa wananunua master ya sinema moja mpya kwa shilingi milioni 10 tu, ambazo utakuta ndio gharama za ktengenezea filamu sasa hapo unabaki na nini?” alihoji.
More Stories
Kocha mkongwe nchini ampigia chapuo Ndayilagije Yanga
Taifa Stars kuingia kambini leo, kuivutia kasi Guinea
Namungo yapaa Morocco kuifuata Raja